Messi:Si rahisi kuwa kwenye fainali nyingine

Argentina itacheza na mshindi kati ya Uruguay na Colombia kwenye fainali ya Copa America

Muhtasari

•Lionel Messi alifunga kwenye nusu fainali kati ya Argentina na Canada na kuiwezesha Argentina kuicharaza Canada 2-0.

•Nusu  fainali ya pili itawahusisha Uruguay na Colombia ,Julai 11  mwendo wa saa tisa asubuhi saa za Afrika Mashariki

Lionel Messi
Image: INSTAGRAM

Nahodha wa Argentina,Lionel Messi ameelezea furaha yake baada ya timu yake kufika kwenye fainali ya kombe la Copa America 2024 baada ya kuiadhibu Canada 2-0. 

Messi alifunga bao lake la kwanza la michuano hiyo katika dakika ya 51 na kuisaidia Argentina kuwa na bao la pili baada ya Julian Alvarez kupachika la kwanza. Kufuatia ushindi huo, Messi mwenye furaha alisema anafurahia ‘vita vyake vya mwisho’ na taifa hilo la Argentina.

“Si rahisi kuwa kwenye fainali nyingine, kushindana tena ili kuwa mabingwa, tunachokipata ni kigumu sana na tunatakiwa kutumia fursa hiyo. Si rahisi kufanya hivi na tunafanya tena," Messi alisema.

Alipoulizwa kuhusu mustakabali wake , alisema kuwa;

Ninajua, kama ilivyo kwa Otamendi, Di María na mimi, kwamba hizi ni vita vya mwisho na tunavifurahia kwa ukamilifu.”

Ushindi huo wa Argentina umewapa fursa nyingine ya kuhakikisha kuwa  wanatetea taji hilo la Copa America baada ya kuishinda  Brazil  1-0 mwaka wa 2021.

Argentina sasa itashiriki katika mpambano wa kilele huko Miami Jumapili ambapo watamenyana na mshindi kati ya  Colombia na Uruguay mechi ambayo imeratibiwa kuchezwa Alhamisi,Julai 11 2024.