Rasmi! Olivier Giroud astaafu soka ya kimataifa

Giroud aliichezea Les Bleus mara 137 na kufunga mabao 57, zaidi ya mchezaji yeyote wa Ufaransa

Muhtasari

•Kocha Didier Deschamps amemtolea sifa kochokocho Giroud na kumtaja kama baadhi ya viongozi kwa klabu hio.

•Giroud atakuwa anaelekea Los Angeles FC  baada ya kandarasi yake kukamilika na klabu ya AC Milan msimu uliopita.

Olivier Giroud
Image: Facebook

Ni rasmi sasa kuwa mshambulizi wa Ufaransa Olivier Giroud amestaafu soka ya kimataifa baada ya Ufaransa kubanduliwa nje ya mashindano ya Euro 2024.

Giroud aliichezea Les Bleus mara 137 na kufunga mabao 57, zaidi ya mchezaji yeyote wa Ufaransa. Kwenye mechi za Euro 2024,Giroud amecheza jumla ya dakika 56 tangu mashindanao yaanze,huko Ujerumani, huku Kolo Muani na Marcus Thuram wakianza mbele yake.

Giroud, 37, alitangaza kustaafu soka ya kimataifa kabla ya michuano hiyo, huku akifanikiwa kuhamia Los Angeles FC baada ya kandarasi yake kukamilika katika klabu ya AC Milan msimu uliopita.

Kocha wa Ufaransa,Didier Deschamps alimpokeza sifa kochokocho  kwa mshambulizi huyo;

"Alikuwa na nyakati nyingi nzuri, lakini pia nyakati ngumu zaidi.Yeye ni mfano wa wachezaji ambao wamekuwa na  maisha marefu, umakini na taaluma. Ingawa alikuwa na wakati mdogo wa kucheza kwenye Euro hii, alikuwa na kikosi kikamilifu. Yeye ni mmoja wa viongozi. Nataka kusema kuwa  amefanya vizuri na ninamshukuru mno."

Giroud alishinda mechi yake ya kwanza mwaka 2011 dhidi ya Marekani, wakati Laurent Blanc alipokuwa kocha.Pia alikuwa kwenye timu iliyopoteza fainali ya Euro 2016.

Vile vile Giroud aliongoza safu ya ushambulizi kwenye kikosi cha Ufaransa kilichoshinda kombe la dunia nchini Urusi japo hakufunga bao lolote. 

Pia alishiriki kwenye kombe la dunia  huko Qatar mnamo 2022 huku akifunga mabao manne wafaransa hao walipotinga fainali na kupoteza kwa Argentina kwa mikwaju ya penalti.

Alipotangaza kustaafu kutoka kwa soka la kimataifa, Giroud alisema bado anahisi kama anaweza kucheza kwa takriban miaka miwili ijayo,kando na umri wake kuyoyoma.

"Nilifikiria kwa makini. Kucheza kila baada ya siku tatu ni ngumu zaidi na zaidi, haswa katika kiwango hiki." Giroud alisema.