Mshtuko huku polisi akimpiga risasi mchezaji wakati wa mechi (+video)

Timu imeonya kuwa itamshtaki polisi aliyempiga risasi na kumjeruhi mlinda mlango wao.

Muhtasari

•Klabu ya Centro Oeste ilishinda mechi hiyo kwa mabao 2-1 kabla ya kutokea kwa mzozo baada ya dakika za mchezo kukamilika.

•Afisa wa polisi alionekana akimpiga risasi ya mpira (plastiki) kipa wa Gremio Anapolis Ramon Souza kufuatia mzozo huo. 

Image: HISANI

Vurugu katika soka ya Brazil ilichukua sura mpya usiku wa kuamkia Alhamisi ambapo afisi wa polisi, huku akijaribu kutuliza mvutano katika mechi kati ya timu mbili za vijana, alipompiga risasi golikipa.

Tukio hilo lilitokea katika mchuano mkali kati ya timu za vijana za Gremio Anapolis na Centro Oestes.Klabu ya Centro Oeste ilishinda mechi hiyo kwa mabao 2-1 kabla ya kutokea kwa mzozo baada ya dakika za mchezo kukamilika, kulingana na gazeti la Brazil, Globo.

Mwishoni mwa mechi kulitokea mvutano, wachezaji wa nyumbani wa Gremio walimvamia mwamuzi, pia kukatokea vita na timu pinzani na ndipo polisi mmoja alipoamua njia nzuri ya kutuliza hali hiyo ni kumpiga risasi mchezaji mmoja.

Afisa huyo wa polisi alionekana akimpiga risasi ya mpira (plastiki) kipa wa Gremio Anapolis Ramon Souza kufuatia mzozo huo. Mchezaji huyo  alibaki na jeraha kwenye paja.

Souza alionekana akichechemea kufuatia tukio hilo la kushangaza, huku klabu yake ikithibitisha kuwa alipata matibabu baada ya kupigwa risasi ya mguu.

Alipigwa na risasi ya plastiki, kwa hivyo maisha yake hayako hatarini, lakini ni wazi kuwa hii ilikuwa kipindi chenye chungu kwa kipa wa Gremio.

Timu hiyo ya Brazil imeonya kuwa itamshtaki polisi aliyempiga risasi na kumjeruhi mlinda mlango wao. Polisi pia wameripotiwa kuanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.