Uchunguzi waendelea kubaini chanzo cha rabsha kati ya mechi ya Argentina na Morocco

Argentina ilipoteza kwa mabao 2-1 mikononi mwa Morocco

Muhtasari

•Mechi hio ilisitishwa kwa takriban masaa mawili baada ya mashabiki kuvamia uwanja,hii ni baada ya Argentina kufunga bao la kusawazisha na kufanya matokeo kuwa 2-2.

•Hata hivyo baada ya ukaguzi wa VAR bao lake Cristian Medina lilikataliwa baada ya mechi kuendelea na matokeo kuishia 2-1 kwa faida ya Morocco.

mashabiki waingia uwanjani kwenye mechi kati ya Argentina na Morocco
mashabiki waingia uwanjani kwenye mechi kati ya Argentina na Morocco
Image: Hisani

Waandalizi wa michezo ya Olimpiki ya Paris wanachunguza kilichosababisha uvamizi wa uwanja wakati wa mechi ya ufunguzi wa mashindano ya soka ya Olimpiki kati ya Argentina na Morocco.

Argentina ilipoteza kwa mabao 2-1 kufuatia ukaguzi wa VAR baada ya mchezo kusimamishwa huku matokeo yakiwa ni 2-2 lakini matokeo ya mwisho yalithibitishwa saa mbili baadaye mchezo ulipoanza tena.

"Mechi ya kandanda kati ya Argentina na Morocco katika Uwanja wa Saint-Etienne ilisitishwa kutokana na uvamizi wa uwanja uliofanywa na watazamaji wachache," waandaaji wa michezo hiyo walisema.

Waliongeza;"Mechi ilianza tena na ikaweza kumalizika salama. Paris 2024 inashirikiana na wadau husika kuelewa sababu na kubaini hatua zinazofaa."

Mchezaji wa Argentina Cristian Medina alifunga bao la kwanza dakika za lala salama na kuokoa kile kilichoonekana kama sare ya 2-2, lakini uamuzi wa kukataa bao la kuotea kufuatia ukaguzi wa VAR ulitolewa takriban saa mbili baada ya mchezo kusimamishwa.

Mara baada ya utaratibu kurejeshwa na timu kuondoka uwanjani kufuatia uvamizi huo ambapo walinzi waliwakimbiza mashabiki kadhaa uwanjani, ilionekana wazi kuwa mechi hiyo ilikuwa haijakamilika bali imesimamishwa.

Timu hizo ziliibuka tena na kumaliza mechi hiyo katika uwanja mtupu, zikicheza kwa dakika tatu na sekunde 15 baada ya VAR kukamilisha ukaguzi wake na kukataa bao hilo, katika mwanzo wa mashindano hayo kwa fujo.

"Kulikuwa na uvamizi mdogo ambao haukupaswa kutokea, lakini ulikuwa wa tabia njema. Mazungumzo yamefanyika kati ya kamati ya maandalizi na FIFA na kila kitu kitarejea katika hali yake ya kawaida," Waziri wa michezo wa Ufaransa Amelie Oudea Castera alisema.

Aliongeza; "Kuna mechi wiki ijayo huko Saint Etienne na kila kitu kitakuwa sawa, ninaahidi."