Ukurasa rasmi wa Shabana FC kwenye Facebook umerejeshwa, miezi 11 baada ya kudukuliwa!

Ukurasa wao rasmi wenye wafuasi zaidi ya 122k ulidukuliwa mwezi Septemba mwaka jana, na sasisho lao la mwisho lilikuwa taarifa kuhusu mechi kati yao na AFC Leopards.

Muhtasari

• Baada ya kudukuliwa kwa ukurasa huo, Shabana FC waliamua kuunda ukurasa mbadala huku taratibu za kukomboa ukurasa rasmi zikiendelea.

• Miezi 11 baadae, ukurasa rasmi umerejea mikononi mwao huku ukurasa mbadala ukiwa tayari umepata zaidi ya wafuasi 54k.

 

SHABANA FC
SHABANA FC

Klabu ya Shabana FC hatimaye imetangaza kukomboa ukurasa wake wa Facebook uliodukuliwa miezi 11 iliyopita.

Shabana FC ilitangaza kurejeshwa kwa ukurasa wao rasmi kupitia ukurasa mbadala kwenye mtandao huo wa kijamii huku ikiwaomba mashabiki wake kuendelea kufuatilia ukurasa huo uliorejeshwa kwa taarifa rasmi kuhusu shughuli za klabu.

“Hatimaye ukurasa rasmi wa kuthibitishwa wa Shabana FC umerudi. Hebu sote tufuate kwa sasisho rasmi za klabu. Msimu mpya mambo mapya,” Shabana walitangaza.

Ukurasa wao rasmi wenye wafuasi zaidi ya 122k ulidukuliwa mwezi Septemba mwaka jana, na sasisho lao la mwisho lilikuwa taarifa kuhusu mechi kati yao na AFC Leopards.

Baada ya kudukuliwa kwa ukurasa huo, Shabana FC waliamua kuunda ukurasa mbadala huku taratibu za kukomboa ukurasa rasmi zikiendelea.

Miezi 11 baadae, ukurasa rasmi umerejea mikononi mwao huku ukurasa mbadala ukiwa tayari umepata zaidi ya wafuasi 54k.

Klabu hiyo ya soka kutoka eneo pana la Gusii inayoshiriki katika ligi kuu ya soka nchini, FKF-PL iliponea shoka la kushushwa daraji, msimu mmoja tu baada ya kupandishwa daraja kutoka ligi pana ya taifa, NSL.

Shabana FC walimaliza msimu katika nafasi ya 14 na pointi 38 mbele ya FC Talanta, Sofapaka, Muhoroni Youth na Nzoia Sugar.

Klabu hiyo inayotajwa kuwa ya tatu humu nchini kwa wingi wa mashabiki baada ya AFC Leopards na Gor Mahia ilisuasua katika sehemu kubwa ya msimu na ilikuja kupata fomu yake mwishoni mwa msimu ambapo kocha Sam Omollo Pamzo aliwasaidia kunusurika kushushwa daraja.