• Alipoulizwa kama uongozi wa klabu ulikuwa umeweka malengo yoyote kwa msimu huu, Maresca alijibu: "Ili tu kuwa na hisia kwamba tunaenda katika mwelekeo sahihi."
Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca amekiri kwamba klabu hiyo ya London Magharibi hawana lengo la kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mpambano wake wa kwanza akiongoza Chelsea kwenye ligi ya premia, Muitaliano huyo alisema kuwa wamiliki wa klabu hiyo wamechagua mkakati wa muda mrefu kupata mafanikio, na wala lengo si kupeleka timu kwenye mabano ya nne bora ifikapo mwisho wa msimu huu.
Maresca alisema: “Ninachoweza kusema ni kwamba hakuna mtu wa klabu aliyeniomba kuirudisha timu kwenye mabano ya 4 bora ili kushiriki Ligi ya Mabingwa mwaka huu.”
Alipoulizwa kama uongozi wa klabu ulikuwa umeweka malengo yoyote kwa msimu huu, Maresca alijibu: "Ili tu kuwa na hisia kwamba tunaenda katika mwelekeo sahihi."
"Hili ni lengo zuri sana tayari wakati mmiliki, wakurugenzi wa michezo, meneja na wachezaji wote wana wazo moja - kwamba tunaenda katika mwelekeo mmoja. Ikiwa sio sasa basi labda inaweza kuwa katika mwezi mmoja, mbili. miezi, katika mwaka mmoja lakini tutafika hivi karibuni."
Tangu kuchukua mikoba ya Roman Abramovich Mei 2022, Todd Boehly na Behdad Eghbali wamewafuta kazi mameneja watatu na kusajili wachezaji 35 ndani ya miaka miwili pekee. Hata hivyo, Maresca amehakikishiwa kuwa hana presha ya kumaliza katika nafasi nne za juu katika msimu wake wa kwanza.
Kocha huyo aliyeisaidia Leicester City kurejea kwenye ligi ya EPL msimu jana, alisema kwamba wamiliki walichagua mkakati wa muda mrefu kupata mafanikio, akifichua kuwa itachukua kati ya miaka 5 hadi 10 kufanikisha hilo.
Chelsea wanatarajiwa kushuka dimbani Jumapili katika mpambano wao wa kufungua msimu dhidi ya bingwa mtetezi, Manchester City.