• “Tore Bobe, karibu kwenye nyumba yako mpya!!🤝 Imethibitishwa, Imetiwa Saini na Kufungwa,” SportPesa waliandika kwenye ukurasa wao wa Facebook.
Klabu ya Shabana FC inayoshiriki katika ligi kuu ya FKF-PL nchini Kenya imeripotiwa kupata mfadhili mpya kwa kampeni ya msimu huu wa mwaka 2024/25.
Kupitia ukurasa wao wa X, Shabana, licha ya kutotoa tangazo rasmi kuhusu ufadhili huo, walionekana wakiwajibu mashabiki waliokuwa wakihoji kuhusu jezi mpya za mfadhili huyo.
Uvumi wa kupata mfadhili mpya ulizuka baada ya kampuni ya Kamari ya SportPesa kuchapisha ujumbe wa kuwakaribisha Shabana kama washirika wapya katika kutangaza chapa yao katika soka.
“Tore Bobe, karibu kwenye nyumba yako mpya!!🤝 Imethibitishwa, Imetiwa Saini na Kufungwa,” SportPesa waliandika kwenye ukurasa wao wa Facebook.
Kupitia X, Shabana walinukuu ujumbe wa SportPesa kuwakaribisha na kusema, “Hapa ndipo.”
Kuhusu suala la Jezi, Shabana walisema kwamba ndio wako katika hatua za lala salama kuchapisha jezi zenye chapa ya SportPesa na pia kuzisafirisha katika maduka rasmi kwa ajili ya kununuliwa na mashabiki.
“Ikiisha tutawasiliana kwa uhakika, tunakamilisha uzalishaji na usafirishaji,” Shabana walijibu.
Itakumbukwa klabu hiyo kutoka eneo la Gusii yenye ushabiki mkubwa ilirudi kwenye ligi msimu uliopita baada ya kuwa nje kwa miaka 17.
Shabana walikuwa wanafadhiliwa na kampuni nyingine ya Kamari, Bang Bet – mfadhili ambaye walimpata msimu jana ukianza.