•Merino amejiunga na klabu hiyo ya Uingereza akitokea Real Sociedad kwa dili yenye thamani ya £27.4m (pamoja na nyongeza za £4.2m).
•Mkurugenzi wa michezo, Edu alieleza furaha ya klabu hiyo kuhusu usajili wa Merino na kusema kwamba atafaa katika kikosi chao.
Klabu ya soka ya Arsenal imethibitisha kumsajili kiungo wa kati wa Uhispania Mikel Merino.
Merino amejiunga na klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza akitokea Real Sociedad kwa dili yenye thamani ya £27.4m (pamoja na nyongeza za £4.2m).
Klabu hiyo inayonolewa na kocha Mikel Arteta ilithibitisha kwamba kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 alisaini mkataba wa muda mrefu ambao unaweza kumweka London kwa miaka minne hadi mitano ijayo.
"Mchezaji wa kimataifa wa Uhispania Mikel Merino amejiunga nasi kutoka kwa Real Sociedad ya La Liga kwa mkataba wa muda mrefu.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 amekuwa kiungo muhimu wa timu ya Sociedad tangu ajiunge na klabu ya Basque mwaka 2018. Katika ya safu yao ya katikati, alicheza mechi 242, akifunga mabao 27 na kusaidia mara 30," Arsenal ilisema katika taarifa.
Mkurugenzi wa michezo wa Arsenal Edu alieleza furaha ya klabu hiyo kuhusu usajili wa Merino na kusema kwamba atafaa katika kikosi chao.
"Tunamkaribisha Mikel na familia yake kwenye klabu, na tunatazamia kumuona akicheza jezi ya Arsenal," Edu alisema.
Kocha Mikel Arteta pia alibainisha kuwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 28 atakuwa kiungo mzuri kwenye kikosi na ataleta uzoefu na ubora mwingi.
“Mikel pia ni mshindi, kutokana na uchezaji wake mzuri katika muda wote wa Euro kusaidia Uhispania kushinda mashindano hayo. Tunayo furaha kumkaribisha Mikel na familia yake kwenye klabu na tunasubiri kuanza kufanya kazi naye," Arteta alisema.
Merino ambaye amekuwa shabiki wa muda mrefu wa Arsenal tangu utotoni atavaa jezi namba 23 na mara moja ataungana na wachezaji wenzake wapya katika Kituo cha Mafunzo cha Sobha Realty.