Kipa Aaron Ramsdale na mshambuliaji Eddie Nketiah wagura Arsenal

Wawili hao tayari wamekubaliana masharti na Southampton na Crystal Palace mtawalia

Muhtasari

•Wanabunduki watapokea pauni milioni 25 na nyongeza ya 5m kutoka kwa Crystal Palace kwa mauzo ya Nketiah.

•Pia watapokea pauni milioni 18 na nyongeza ya 7m kutoka kwa Southampton kwa uhamisho wa kipa Aaron Ramsdale.

Eddie Nketiah na Aaron Ramsdale
Image: HISANI

Kipa Aaron Ramsdale na mshambuliaji Eddie Nketiah wanaripotiwa kukaribia kuondoka katika klabu ya soka ya Arsenal.

Ripoti kutoka Ulaya zinaonyesha kuwa wachezaji hao wawili wa timu ya taifa ya Uingereza tayari wamekubaliana masharti na Southampton na Crystal Palace mtawalia. Klabu hizo mbili pia zimefanya makubaliano ya uhamisho ya wawili hao na Arsenal.

Inaripotiwa kuwa wanabunduki watapokea pauni milioni 25 na nyongeza ya 5m kutoka kwa Crystal Palace kwa mauzo ya Nketiah.

Klabu hiyo pia itapokea pauni milioni 18 na nyongeza ya 7m kutoka kwa Southampton kwa uhamisho wa kipa Aaron Ramsdale.

 

Wachezaji hao wawili wanatarajiwa kukamilisha uhamisho kutoka kwa klabu hiyo ya Kaskazini mwa London wiki hii huku vikao vya vipimo vya afya vikiwa tayari vimepangwa.

Mapema wiki hii, kiungo Fabio Viera alikamilisha uhamisho wake wa mkopo kurudi katika klabu yake ya zamani ya Porto katika juhudi za kumpa muda zaidi wa kucheza.

Klabu hiyo inayoongozwa na kocha Mikel Arteta pia ilimuuza kiungo wa kati Charlie Patino kuenda Deportivo La Coruna kwa pauni 1m.

Wachezaji wawili wapya, beki Ricardo Callafiori na kiungo Mikel Merino, tayari wamejiunga na klabu hiyo katika juhudi za kuimarisha kikosi.