"Natarajia mechi 100 za EPL kuchezwa 10 dhidi ya 11!" Arteta azungumzia kadi nyekundu ya Trossard

"Natarajia sasa mechi 100 za Ligii Kuu kuchezwa wachezaji 10 dhidi ya 11, au 10 dhidi ya tisa. Ngoja tuone,” Arteta alisema.

Muhtasari

•Trossard alionyeshwa kadi ya pili ya njano na kadi nyekundu muda mfupi kabla ya kipindi cha mapumziko kwa kuupiga mpira nje.

•Arteta alizungumzia kutoridhika kwake na kutolewa nje kwa Trossard na akaelezea wasiwasi wake kuhusu wingi wa kadi zinazotolewa.

Mikel Arteta, meneja wa Arsenal.
Mikel Arteta, meneja wa Arsenal.
Image: HISANI

Kocha Mikel Arteta alionyesha kutoridhika kwake baada ya mshambuliaji Leandro Trossard kutolewa nje kwa kadi nyekundu wakati Arsenal ilipotoka sare ya 2-2 dhidi ya Manchester City kwenye Uwanja wa Etihad Jumapili jioni.

Winga huyo wa Ubelgiji alionyeshwa kadi ya pili ya njano na kadi nyekundu muda mfupi kabla ya kipindi cha mapumziko kwa kuupiga mpira nje. Awali alikuwa ameonyeshwa kadi nyingine ya njano baada ya kufanya dhambi.

Akizungumza na BBC baada ya mechi hiyo ya kusisimua, Arteta alieleza fahari yake kwa timu yake baada ya kuweza kutopoteza licha ya kuwa na wachezaji wachache uwanjani.

"Ninajivunia timu. Tulicheza mchezo katika mazingira magumu, dhidi ya timu bora zaidi duniani. Baada ya kile kilichotokea, tulikwenda 2-1-ilikuwa hadithi tofauti, na sipendi kutoa maoni kuhusu [kadi nyekundu ya Trossard]. Tayari ni muujiza tulicheza dakika 56 pale Etihad tukiwa na watu 10. Ni jambo la kushangaza tumefanya," Arteta alisema.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 42 alidokeza zaidi kutoridhika kwake na kutolewa nje kwa Trossard na akaelezea wasiwasi wake kuhusu wingi wa kadi zinazotolewa.

"Ni dhahiri kilichotokea walipofanya uamuzi huo, lakini haifai maoni yangu. Sitaki kuharibu kitu kingine chochote nje ya uwanja. Ni mara ya pili. Natarajia [sasa] mechi 100 za Ligii Kuu kuchezwa wachezaji 10 dhidi ya 11, au 10 dhidi ya tisa. Ngoja tuone,” alisema.

Aliongeza, "Nadhani ni dhahiri sana kile watu wanachofikiria kuhusu kadi nyekundu. Sio kazi yangu kuja hapa na kuhukumu kilichotokea. Kazi yangu ni kuishi katika mojawapo ya mazingira magumu zaidi yaliyopo kwenye soka kwa dakika 55 na kujaribu kufanya mambo ili kuendelea kuishi.

Kadi ya Trossard siku ya Jumapili ni mara ya pili katika wiki za hivi karibuni kwa mchezaji wa Arsenal kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa tukio kama hilo, baada ya Declan Rice kuonyeshwa kadi nyekundu kwenye pambano dhidi ya Brighton.