
Mchezaji wa Kimataifa wa Uingereza Marcus Rashford alikamilisha uhamisho kutoka Manchester United kwenda Aston Villa Jumapili jioni.
Villa ilithibitisha kumsajili winga huyo mwenye umri wa miaka 27 kwa mkopo kupitia kurasa zao rasmi za mitandao ya kijamii.
"Aston Villa ina furaha kutangaza kumsajili kwa mkopo Marcus Rashford kutoka Manchester United," Villa ilisema katika taarifa kwenye X.
Rashford anaripotiwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu katika Villa Park siku ya Jumapili kabla ya kujiunga na kikosi hicho kinachonolewa na Unai Emery.
Mshambulizi huyo ataichezea Villa kwa muda uliosalia wa msimu wa 2024/25 na klabu hiyo yenye maskani yake Birmingham itagharamia 75% ya mshahara wake wakati huo. Kwa kawaida anapokea mshahara wa Pauni 325,000 kwa wiki katika Man United.
Villa walikabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa vilabu vingine kupata saini ya winga huyo mwenye umri wa miaka 27 na watakuwa na chaguo la kumnunua kabisa kwa pauni milioni 40 baada ya kumalizika kwa muda wa mkopo mwezi Juni.
"Ningependa kuwashukuru Manchester United na Aston Villa kwa kufanikisha mpango huu wa mkopo," Rashford alisema baada ya kukamilisha uhamisho huo.
"Nilikuwa na bahati kuwa na vilabu vichache vilivyonikaribia lakini Aston Villa ulikuwa uamuzi rahisi kufanya- nafurahia sana jinsi Aston Villa imekuwa ikicheza msimu huu, na matarajio ya wasimamizi," aliongeza.
Pia alieleza kuhusu kiasi gani anataka kucheza tena baada ya kuwekwa nje na kocha wa Man United, Ruben Amorim katika wiki kadhaa zilizopita.
"Nawatakia kila la heri Manchester United kwa kipindi kizima kilichosalia," alisema.