Alexandre Lacazette ajiunga na Lyon baada ya kuondoka Arsenal

Muhtasari

•Lacazette anarejea katika klabu hiyo ya Ufaransa kwa mkataba wa miaka mitatu hadi Juni 2025.

Image: BBC

Mshambulizi wa Arsenal Alexandre Lacazette amesajiliwa tena Lyon kwa uhamisho wa bila malipo - miaka mitano baada ya kuondoka na kujiunga na The Gunners kwa rekodi ya klabu wakati huo ya £46.5m.

Lacazette anarejea katika klabu hiyo ya Ufaransa kwa mkataba wa miaka mitatu hadi Juni 2025.

Mshambuliaji huyo wa Ufaransa alifunga mabao 54 katika mechi 158 za Ligi ya Primia akiwa na Arsenal na kusaidia The Gunners kushinda fainali ya Kombe la FA 2020.

Akizungumza na Canal Plus mwezi Aprili, Lacazette alisema "hajawahi kukata mawasiliano" na klabu ya nyumbani ya Lyon.

Lyon walisema "walijivunia sana na wana furaha sana" kutangaza kurejea kwa Lacazette katika klabu aliyojiunga nayo akiwa na umri wa miaka 12, na kuongeza kuwa mkataba "umekuwa kipaumbele cha klabu kwa miezi kadhaa".

Lacazette, 31, alipanda timu za vijana huko Lyon na kufunga mabao 129 katika mechi 275 katika mashindano yote baada ya kuingia kwenye kikosi cha kwanza katika kampeni za 2009-10.

Alisajiliwa na Arsene Wenger mwaka wa 2017 kwa mkataba huo - hadi £52.6m na nyongeza - kupita £42.4m Arsenal ililipa Real Madrid kwa Mesut Ozil mwaka 2013.