Babake Erling Halaand apendekeza Arsenal kushinda ligi baada ya kutwaa Community Shield

Arsenal ilishinda Kombe la Community Shield Jumapili jioni baada ya kuwapiga Man City kwenye Uwanja wa Wembley.

Muhtasari

•Erling Halaand alionyesha mchezo hafifu dhidi ya Arsenal siku ya Jumapili jioni hadi kocha wa Mancity Pep Guardiola alilazimika kumtoa.

•Alfie Halaand aliwapongeza vijana wa Mikel Arteta kwa utani na kupendekeza watashinda kombe la EPL 2023/24.

na babake Alfie Halaand baada ya Man City kushinda kombe la EPL 2022/23.
Erling Halaand na babake Alfie Halaand baada ya Man City kushinda kombe la EPL 2022/23.
Image: HISANI

Klabu ya Soka ya Arsenal ilishinda Kombe la Community Shield siku ya Jumapili jioni baada ya kuwapiga washindi wa Ligi ya Mabingwa, EPL na FA msimu uliopita, Manchester City kwenye Uwanja wa Wembley.

Wanabunduki waliwanyorosha Man City kwa mikwaju ya penalti na kushinda taji lao la kwanza msimu wa 2023/24 baada ya dakika 90 za kawaida kumalizika kwa sare ya 1-1. Walifunga penalti nne huku vijana wa Pep Guardiaola wakifunga moja tu kati ya majaribio yao matatu.

Kufuatia ushindi huo, maoni tofauti yaliibuka mitandaoni ya kijamii huku baadhi ya mashabiki wa soka wakiipongeza klabu hiyo yenye maskani yake jijini London huku wengine wakikejeli ushindi huo. Mashabiki pia walichambua na kutoa maoni kuhusu mchezo wa Manchester City kufuatia kipigo hicho.

Akaunti ya Twitter @TrollFootball ilitoa maoni kuhusu mchezo hafifu wa mshambuliaji matata wa Man City Erling Haaland katika mchuano huo na pia katika mechi za hivi majuzi za kabla ya msimu mpya.

"Mashabiki wa Ligi ya Premia baada ya kuona mchezo mbaya wa Haaland katika mechi ya Community Shield lakini wakumbuke alifanya hivyo msimu uliopita," yalisomeka maoni ya @TrollFootball na kuambatanishwa na video ya kocha wa Southampton Ralph Hasenhuttl akisherehekea baada ya kuchukua uongozi wakati wa mchezo wao dhidi ya wanabunduki msimu uliopita.

Miongoni mwa watu waliotoa maoni kwenye video hiyo si mwingine ila baba mzazi wa Erling Haaland, Alfie Halaand ambaye aliwapongeza vijana wa Mikel Arteta kwa utani na kupendekeza watashinda kombe la EPL 2023/24.

"Mmefanya vizuri Arsenal, ushindi mkubwa. Lazima uwe vipenzi vya ligi sasa,” Alfie Halaand alisema.

Mshambuliaji Erling Halaand alionyesha mchezo hafifu dhidi ya Arsenal siku ya Jumapili jioni hadi kocha wa Mancity Pep Guardiola alilazimika kumtoa na kumbadilisha na chipukizi Cole Palmer katika dakika ya 64.

Palmer alifunga bao zuri dakika 13 baadaye baada ya kuingia na kuipa City bao la uongozi kabla ya Arsenal kusawazisha katika dakika za nyongeza kuelekea mwisho wa mechi.

Hata hivyo, matumaini ya Mancity kunyanyua taji la kwanza msimu huu yalikufa baada ya nahodha Kevin De Bruyne na Rodri kukosa penalti zao huku Martin Odegaard wa Arsenal, Leandro Trossard, Bukayo Saka na Fabio Vera wakifunga majaribio yao yote.