Christiano Ronaldo: Man United imenisaliti, simheshimu kocha Erik Ten Hag

Mshambulizi huyo amekiri kuwa hana raha katika klabu hiyo inayoshabikiwa sana.

Muhtasari

•Raia huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 37 aliweka wazi kuwa yeye ni mtu anayepaswa kuheshimiwa na kusikilizwa.

•Alisema hana heshima yoyote kwa kocha wa United, Erik teg Hag,  kwani pia yeye  hajaonyesha heshima kwake.

Amefichua kuwa hana raha katika klabu hiyo ya Premier league.
Mshambulizi wa Manchester United Christiano Ronaldo. Amefichua kuwa hana raha katika klabu hiyo ya Premier league.
Image: GETTY IMAGES

Mshambulizi wa Manchester United Christiano Ronaldo amevunja ukimya kuhusu matatizo yake na klabu hiyo ya Premier League.

Katika mahojiano na mwanahabari Piers Morgan, Mreno huyo aliweka wazi kuwa hana raha katika klabu hiyo inayoshabikiwa sana.

Christiano alidai kuwa baadhi ya watu katika uongozi wa klabu hiyo akiwemo kocha Erik Ten Hag  wamekuwa wakijaribu kumtimua nje kwa nguvu tangu msimu uliopita, jambo ambalo linamfanya ahisi amesalitiwa.

"Wamekuwa wakijaribu kunitoa, sio kocha tu. Pia watu wengine watatu hivi kwenye klabu. Nilihisi nimesalitiwa," alisema.

Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 37  alisema alihisi kusalitiwa kwani yeye ni mtu anayepaswa kuheshimiwa na kusikilizwa.

Alipoulizwa kwa nini viongozi wakuu wa klabu walikuwa wakijaribu kumfukuza, mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ureno alijibu: "Kusema kweli, sijui. Sijali. Watu wanapaswa kusikia ukweli. Ndiyo, nahisi kusalitiwa. Baadhi ya watu hawakutaka niwe hapa sio mwaka huu tu, bali mwaka jana pia."

Aidha aliweka wazi kuwa hana heshima yoyote kwa kocha wa United, Erik teg Hag,  kwani pia yeye  hajaonyesha heshima kwake.

"Simheshimu Erik ten Hag kwa sababu haonyeshi heshima kwangu. Ikiwa huniheshimu, sitawahi kukuheshimu," alisema.

Christiano pia aliibua madai kwamba hakujakuwa na mabadiliko yoyote katika klabu ya Manchester United tangu kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu, Sir Alex Ferguson takriban miaka tisa iliyopita.

"Nilidhani nikirudi ningeona vitu tofauti; teknolojia, miundombinu. Kwa bahati mbaya, tunaona vitu vingi ambavyo nilizoea kuona nikiwa na miaka 21, 22, 23. Ilinishangaza sana," alisema.

Alikosoa uteuzi wa Ralf Rangnick  kama kocha wa muda baada ya kutimuliwa kwa Ole Gunnar Solskjær mwaka jana.

Christiano alijiunga tena na Mashetani Wekundu Agosti 2021 na kumaliza kama mfungaji bora wao katika mashindano yote msimu uliopita akiwa na mabao 24.