Darwin Nunez, wenzake wa Uruguay walimana ngumi na mashabiki wa Colombia baada ya kichapo (+video)

Nunez aliyejawa na hisia kali alizuiliwa na walinzi wakati yeye na wachezaji wenzake walichukua mambo mikononi mwao.

Muhtasari

•Nunez aliruka kwenye eneo la kutazamia mpira na kuwarushia ngumi mashabiki katika pambano lisilo la kawaida baada ya mechi dhidi ya Colombia.

•Wachezaji wa Uruguay walijitosa kwenye umati kusaidia familia na marafiki waliokuwa wameketi nyuma ya benchi ya timu. 

katika vita na mashabiki wa Colombia
Darwin Nunez katika vita na mashabiki wa Colombia
Image: HISANI

Nyota wa Liverpool na Uruguay, Darwin Nunez aliruka kwenye eneo la kutazamia mpira na kuwarushia ngumi mashabiki katika pambano lisilo la kawaida baada ya mechi dhidi ya Colombia ambapo Uruguay ilitolewa kwenye michuano ya Copa America usiku wa kuamkia Alhamisi.

Hasira zilipamba moto kati ya mataifa hayo mawili baada ya kipyenga cha mwisho, huku Colombia ikipata ushindi mwembamba wa 1-0 kutokana na bao la kichwa la Jefferson Lerma dakika ya 39. Baada ya mzozo ndani ya uwanja kuisha, wachezaji wa Uruguay waliingia kwenye eneo la mashabiki,

Nunez aliyejawa na hisia kali alizuiliwa na maafisa wa usalama wakati yeye na wachezaji wenzake walichukua mambo mikononi mwao.

Kanda za video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 akiwa na wachezaji wenzake wakiwemo Jose Gimenez na Ronald Araujo huku matukio yakigeuka kuwa mabaya baada ya filimbi ya mwisho.

Nyota huyo wa Liverpool baadaye alionekana akimkumbatia mwanawe mdogo uwanjani, ambaye huenda alinaswa na matukio hayo yasiyo ya kawaida.  Nyota wa Barcelona Ronald Araujo pia alihusika, huku maelfu ya mashabiki wakirekodi ugomvi huo kwenye simu zao kwa kutoamini.

Maafisa wa Usalama kisha waliingia ili kutenganisha pande zote mbili, na kujaribu kuwaongoza wachezaji wa Uruguay kwenye chumba cha kubadilishia nguo haraka iwezekanavyo.

Kulingana na stesheni ya Uruguay El Pais, wachezaji wa Uruguay walijitosa kwenye umati kusaidia familia na marafiki waliokuwa wameketi nyuma ya benchi ya timu. Kukiwa na idadi kubwa ya watu wengi wa Colombia ndani ya uwanja, wapendwa wa nyota wa Uruguay walikuwa wakinyanyaswa.

Baada ya tukio hilo, Gimenez alisema kwenye runinga baada ya tukio hilo kwamba familia za wachezaji hao - waliokuwa wamekaa karibu na mashabiki - 'walighadhabishwa' na mashabiki walevi, na kwamba walijitokeza kuwatetea.

'Hii ni aibu, hakukuwa na afisa mmoja wa polisi wa kuwadhibiti. Ilitubidi kwenda kutetea vyetu kwa sababu tu hawawezi kudhibiti unywaji wao,' alisema.

Shirika lililoandaa mashindano, CONMEBOL litapitia tukio hilo kabla ya fainali ya Copa America Jumapili, ambapo Colombia itakutana na Argentina mjini Miami. Colombia wako kwenye mbio nzuri ya michezo 28 bila kushindwa na hawajapoteza kwa zaidi ya miaka miwili, lakini watakuwa chini ya Argentina.