David de Gea aomba radhi baada ya kuruhusu mabao 7 wavuni

De Gea amewataka wote katika United kusahau yaliyopita na kuangazia tu mechi zilizo mbele yao.

Muhtasari

•David de Gea ametoa taarifa ya kuomba radhi baada ya United kupata kichapo cha mbwa kutoka kwa Liverpool siku ya Jumapili jioni.

•De gea ameitaja mechi hiyo ya kukumbukwa kuwa kipindi kibaya kwa klabu na mashabiki na kuapa kwamba haitajirudia tena.

Image: HISANI

Mlinda lango wa Manchester United, David de Gea ametoa taarifa ya kuomba radhi baada ya klabu hiyo kupata kichapo cha mbwa kutoka kwa Liverpool siku ya Jumapili jioni.

Mashetani Wekundu walipata kipigo cha aibu kwenye Uwanja wa Anfield siku ya Jumapili huku mabao saba yakipita wavuni bila wao kupata nafasi hata ya kufunga angalau bao moja la kufuta machozi.

De gea ameitaja mechi hiyo ya kukumbukwa kuwa kipindi kibaya kwa klabu na mashabiki na kuapa kwamba haitajirudia tena.

"Huu ulikuwa wakati mbaya kwetu na matokeo haya hayapaswi kutokea, haswa na safari ambayo sote tuko," alisema.

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Uhispania sasa amewataka watu wote katika Manchester United kusahau yaliyopita na kuangazia tu mechi chungu nzima ambazo zipo mbele yao kabla ya msimu kuisha.

"Tuna wajibu kwa klabu hii, jukumu la kuwakilisha beji lakini tuna nafasi nyingi za kuangalia mbele, michezo mingi inakuja kwa kasi na tunapaswa kuzingatia hii,"

United walipoteza kwa mara ya 6 msimu huu kwa njia ya kufedhehesha zaidi Jumapili jioni. Kipigo hicho kuliwaacha katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 49 na kuathiri mbio zao za kuwania ubingwa wa EPL.

Washambulizi Cody Gakpo, Mohammed Salah na Darwin Nunez walifunga mabao mawili kila mmoja wakati wa mchuano huo wa kusisimua huku Mbrazil Roberto Firmino ambaye aliingia kama mchezaji wa akiba katika kipindi cha pili akifunga ushindi wa kihistoria wa Liverpool kwa bao maalum.

Ushindi wa Jumapili jioni ndio ushindi mkubwa zaidi kwa Liverpool dhidi ya Manchester United katika historia ya EPL.