Euro 2024: Lamine Yamal wa miaka 16 asaidia Uhispania kupiga Ufaransa na kutinga fainali

Yamal alitunukiwa taji la mchezaji bora wa mechi huku Uhispania ikitoka nyuma na kuipiga Ufaransa.

Muhtasari

• Ufaransa walikuwa wameanza mechi vizuri sana huku mshambuliaji Kolo Muani akiwapatia bao la kwanza katika dakika ya 9.

•Mechi ya nusu fainali kati ya Uholanzi na Uingereza itachezwa mwendo wa saa nne usiku wa Jumatano.

Winga Lamine Yamal
Image: TWITTER// EURO 2024

Kinda wa Barcelona mwenye umri wa miaka 16, Lamine Yamal alitunukiwa taji la mchezaji bora wa mechi huku Uhispania ikitoka nyuma na kuipiga Ufaransa katika mechi ya nusu fainali ya Euro 2024.

Washindi wa Kombe la Dunia 2018, Ufaransa walikuwa wameanza mechi vizuri sana huku mshambuliaji wa PSG Randal Kolo Muani akiwapatia bao la kwanza katika dakika ya 9.

Ilikuwa katika dakika ya 21 ambapo Lamine Yamal alipata nafasi, akaitumia vyema, na kufunga bao zuri lililompita kipa Mike Maignan wa Ufaransa.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 16 aliendelea kucheza mchezo wa kuvutia na alicheza jukumu kubwa katika bao la pili la Uhispania lililofungwa na Dani Olmo katika dakika ya 25.

Katika zaidi  ya dakika 65 zilizofuata za mechi hiyo ilikuwa pambano kubwa, huku timu zote zikijaribu kupata bao ili kuona nani atatinga fainali.

Licha ya nafasi nyingi zilizotengenezwa, si Uhispania wala Ufaransa waliofunga bao lingine hadi mwisho wa mechi iliyochezwa kwa dakika 90+5.

Uhispania sasa wanasubiri kujua watakutana na nani katika fainali ya michuano hiyo kati ya Uingereza na Uholanzi zinazocheza leo usiku, Julai 10.

Mechi ya nusu fainali kati ya Uholanzi na Uingereza itachezwa mwendo wa saa nne usiku wa Jumatano.

Baada ya kukamilika kwa mechi za nusu fainali leo, washindi wawili watamenyana katika fainali itakayochezwa Jumapili, Julai 14.