Ghost Mulee atoa ubashiri wake wa Kombe la Dunia na EPL

Mtangazaji Ghost ameipigia upato timu ya taifa ya Brazil kunyanyua Kombe la Dunia.

Muhtasari

•Mtangazaji huyo alisema timu hizo mbili za Amerika Kusini zina vikosi vizuri ambavyo vinaweza kuzipa wakati mgumu timu nyingine.

•Ghost alibashiri kuwa  klabu ya  Manchester City itaibuka mshindi wa Premier League kwa mara nyingine.

ndani ya studio za Radio Jambo.
Mtangazaji Jacob Ghost Mulee ndani ya studio za Radio Jambo.

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob 'Ghost' Mulee ameipigia upato timu ya taifa ya Brazil kunyanyua Kombe la Dunia.

Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars pia amebashiri kuwa  timu ya Argentina  itatamba sana katika mashindano yanayotarajiwa kuanza Novemba 20.

Katika mahojiano na mwandishi huyu, Ghost alisema timu hizo mbili za Amerika Kusini zina vikosi vizuri ambavyo vinaweza kuzipa wakati mgumu timu nyingine.

"Pia huwezi kufutilia mbali Mjerumani. Huwa ni mjanja sana katika mechi za kimataifa. Ubelgiji walifanya vizuri katika mashindano ya  Kombe la Dunia yaliyopita. Ufaransa wana majeraha mengi kwa hivyo itakuwa ni shinda kwao kuweza kunawiri," alisema.

"Brazil huenda ikaingia fainali. Argentina huenda akatatiza. Pia timu za Europa usizipuuzilie kwa sababu huwa wanashinda wengine kwa mipangilio."

Ghost alisema, kati ya mataifa matano ya Afrika yanazoshiriki katika shindano hilo, Senegal ina uwezekano mkubwa wa kusonga mbali zaidi. Alisema kupatikana kwa Sadio Mane kutasaidia sana timu ya taifa ya taifa hilo la Afrika Magharibi.

"Cameroon huwa na matatizo yake. Ghana pia huenda wakatatiza," alisema

Mtangazaji mwenza huyo wa shoo ya asubuhi alisema hali ya hewa ya kipekee nchini Qatar itacheza nafasi kubwa katika kuamua matokeo. Alisema itakuwa changamoto kubwa kwa timu zote zinazoshiriki Dimba la Dunia kutokana na kwamba si nyingi zilizowahi kucheza mashindano ya kimataifa katika mazingira  kama hayo.

Alidokeza kuwa sheria kali za kidini nchini Qatar hazitaathiri Kombe la Dunia. Alisema  kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba mhemko ambao huambatana na Kombe hilo  bado utashuhudiwa.

Kwenye Ligi ya Uingereza, mkufunzi huyo mahiri alibashiri kuwa  klabu ya  Manchester City itaibuka mshindi kwa mara nyingine.

"Arsenali pia itakuwa top 4, Manchester United pia, Newcastle inababaisha lakini huenda ikateleza. Chelsea pia imefanya vizuri na kocha wao mpya," alisema.

"Naweza nikasema; Man City, Arsenali, Man United na Chelsea," alisema.

Kwenye Champions League, Ghost alizipatia upato Real Madrid na Bayern Munich.