Kwa nini Mashetani Wekundu hawatapinga kadi nyekundu ya Casemiro

Mchezaji huyo atakosa mechi nne baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwa mara ya pili msimu huu.

Muhtasari

•Mashetani Wekundu wameamua kutochukua hatua hiyo kwa kuwa hawaamini wanaweza kubatilisha uamuzi wa refa Antony Taylor.

Mchezaji wa United, Casemiro
Image: HISANI

Klabu ya Manchester United imechagua kutokata rufaa dhidi ya kadi nyekundu iliyoonyeshwa kwa kiungo wa kati Carlos Henrique Casimiro almaarufu Casemiro wakati wa mchuano wao na Southampton siku ya Jumapili.

Vyombo vya habari vya  nchi ya Uingereza vimeripoti kwamba Mashetani Wekundu wameamua kutochukua hatua hiyo kwa kuwa hawaamini wanaweza kubatilisha uamuzi wa refa Antony Taylor.

Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Brazil  sasa atakosa michuano minne za klabu hiyo baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu kwa mara ya pili msimu huu. Atakosa mechi ya Kombe la FA dhidi ya Fulham pamoja na mechi za ligi kuu dhidi ya Newcastle, Brentford na Everton.

Siku ya Jumapili, meneja wa Man United, Erik Ten Haag alionyesha kutoridhishwa na uamuzi wa refa dhidi ya Casemiro huku akilalamika kwamba alikuwa ametolewa uwanjani mara mbili ndani ya wiki chache.

"Casemiro amecheza zaidi ya mechi 500 barani Ulaya. Hajawahi kuwa na kadi nyekundu. Na sasa, ni nini? Katika mechi chache na michezo 20 kwa jumla kwenye Ligi Kuu, amepewa kadi nyekundu mbili," alisema.

Kipa David de Gea pia alionyesha kutoridhishwa na uamuzi huo lakini akaweka wazi kuwa klabu hiyo itaweza kukabiliana na hali hiyo.