Rasmi! Gabriel Jesus ajiunga na Wanabunduki kutoka Man City

Ametia saini mkataba wa miaka mitano.

Muhtasari

•Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, Jesus anaripotiwa liigharimu klabu hiyo pauni milioni 45 (Ksh 6.4B).

•Jesus ametia saini mkataba wa miaka mitano na atavalia jezi nambari 9 ambayo ilimilikiwa na Lacazette hapo awali.

katika uwanja wa Emirates baada ya kujiunga na Arsenal
Mshambuliaji Gabriel Jesus katika uwanja wa Emirates baada ya kujiunga na Arsenal
Image: TWITTER// ARSENAL

Wanabunduki wametangaza usajili wa mshambuliaji matata Gabriel Jesus kutoka Manchester City.

Habari za kusajiliwa kwa Jesus zilitangazwa Jumatatu asubuhi kupitia tovuti rasmi na kurasa za mitandao ya kijamii za Arsenal.

"Gabriel Jesus amesajiliwa kutoka Manchester City kwa mkataba wa muda mrefu," Taarifa ya Arsenali ilisoma.

Mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Brazil ametia saini mkataba wa miaka mitano na Wanabunduki.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uingereza, Jesus anaripotiwa liigharimu klabu hiyo pauni milioni 45 (Ksh 6.4B).

Gabriel ,25, atavalia jezi nambari 9 ambayo awali ilimilikiwa na Alexandre Lacazette ambaye aliondoka mwezi jana na kujiunga na Lyon.

Amejiunga na Arsenal baada ya kuchezea City kwa kipindi cha miaka mitano ambapo alifunga mabao 95 katika mechi 236 alizoshiriki.Hapo awali aliwahi kuchezea Palmeiras ya Brazil.

Katika tangazo la usajili wa Jesus, Mkurugenzi wa ufundi katika Arsenal Edu Gaspar alisema  klabu hiyo inafurahia sana usajili wa mshambuliaji huyo.

"Gabriel ni mchezaji ambaye ametuvutia kwa muda mrefu sasa. Ana umri wa miaka 25 na mchezaji wa kimataifa wa Brazil ambaye ameonyesha mara kwa mara kuwa ni mchezaji wa kiwango cha juu sana. Tunatarajia kumuona akijiunga na wachezaji wenzake wapya kabla ya msimu mpya. Sote tunamkaribisha Gabriel Arsenal." Edu alisema.

Uhamisho wa mshambuliaji huyo unatarajia kukamilika kwa kufuatilia taratibu za udhibiti zilizowekwa.