Thibaut Courtois akataa kuichezea nchi yake ya Ubelgiji, afichua sababu

Aliweka wazi kuwa hana imani na Tedesco na hawezi tena kucheza chini yake kuendelea mbele.

Muhtasari

•Aliwaomba radhi mashabiki wa timu ya Ubelgiji akieleza kuwa matukio yaliyojiri kati yake na kocha Domenico Tedesco yamemfanya achukue uamuzi huo mgumu.

•Kipa huyo wa zamani wa klabu ya Chelsea alisema kuwa yuko tayari kuchukua jukumu la uamuzi wake.

Thibaut Courtois
Image: HISANI

Mlinda mlango wa Real Madrid Thibaut Courtois ametangaza kuwa hataweza tena kutoa huduma zake kwa timu yake ya taifa ya Ubelgiji, angalau kwa sasa.

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, kipa huyo mwenye umri wa miaka 32 aliwaomba radhi mashabiki wa timu ya taifa ya Ubelgiji akieleza kuwa matukio yaliyojiri kati yake na kocha Domenico Tedesco yamemfanya achukue uamuzi huo mgumu.

Aliweka wazi kuwa hana imani na Tedesco na hawezi tena kucheza chini yake kuendelea mbele.

"Nataka kuhutubia mashabiki wa Ubelgiji na wafuasi wa timu yetu ya taifa. Ninahisi upendo mkubwa na fahari katika kuwakilisha nchi yangu uwanjani, na vile vile kila mmoja wenu anayesapoti Mashetani Wekundu.

 Najisikia bahati kuwa nimepata heshima ya kuvaa jezi ya taifa. Hata katika ndoto zangu kubwa zaidi, sikuweza kufikiria kuwa nina uwezo wa kufanya hivyo zaidi ya mara 100,” Courtois alisema katika taarifa iliyoandikwa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Aliongeza, “Kwa bahati mbaya, kufuatia matukio na kocha na baada ya kutafakari sana, nimeamua kutorejea katika timu ya taifa ya Ubelgiji chini ya usimamizi wake. "

Kipa huyo wa zamani wa klabu ya Chelsea alisema kuwa yuko tayari kuchukua jukumu la uamuzi wake akibainisha kuwa tayari ameshafanya mazungumzo na shirikisho la soka nchini humo, na wamekubali uamuzi wake.

"Katika suala hili, ninakubali sehemu yangu ya jukumu. Walakini, nikitazama mbele, ukosefu wangu wa imani kwake haungechangia kudumisha hali ya lazima ya ukarimu. Shirikisho, ambalo nimekuwa na mazungumzo nalo mara kadhaa, linakubali msimamo wangu na sababu zilizonifanya nifikie uamuzi huu mchungu lakini thabiti,” alisema.

"Najuta kuwakatisha tamaa baadhi ya mashabiki, lakini nina hakika kwamba hii ni hatua bora kwa Ubelgiji, kwani inafunga mjadala na kuruhusu timu kuzingatia malengo yake. Asante kwa sapoti yako usiyoyumba, upendo na kuelewa kwako,” alimalizia kwa kusema.

Courtois alianza kuichezea timu yake ya taifa mwaka 2011, akiwa na umri wa miaka 19. Hata hivyo aliachwa nje ya kikosi cha Ubelgiji wakati wa mashindano ya hivi majuzi ya Euro 2024 nchini Ujerumani.