Tottenham Hotspurs yamchukua kocha wa Celtic, Ange Postecoglou

Postecoglou anajiunga na klabu hiyo ya Uingereza kutoka Celtic ya Australia.

Muhtasari

•Katika taarifa ya siku ya Jumatano, Spurs walitangaza kwamba Postecoglou ametia saini mkataba wa miaka minne.

•Daniel Levy alimsifia mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Australia na kudokeza kwamba analeta msisimko mpya.

Kocha Mpya wa Tottenham Ange Postecoglou
Image: HISANI

Klabu ya Tottenham Hotspurs imetangaza uteuzi wa Ange Postecoglou kama kocha wake mkuu mpya.

Katika taarifa ya siku ya Jumatano, Spurs walitangaza kwamba Postecoglou ametia saini mkataba wa miaka minne.

"Sasa kwa kuwa msimu na mashindano yote ya kombe la nyumbani yamekamilika, tunayo furaha kutangaza uteuzi wa Ange Postecoglou kama Kocha wetu Mkuu mpya wa Timu ya Kwanza. Akiwa Mwaustralia wa kwanza kusimamia Ligi Kuu, Ange atajiunga nasi tarehe 1 Julai kwa kandarasi ya miaka minne," taarifa ya Tottenham ilisoma.

Postecoglou anajiunga na klabu hiyo ya Uingereza kutoka Celtic ya Australia.

"Tutatangaza kikosi cha ukufunzi cha Ange' katika wakati mwafaka," taarifa ilisoma.

Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy alimsifia mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Australia na kudokeza kwamba analeta msisimko mpya katika klabu hiyo ambayo ilimaliza katika nafasi ya nane kwenye EPL.

"Ana rekodi nzuri ya kukuza wachezaji na kuelewa umuhimu wa kiungo kutoka akademi - kila kitu ambacho ni muhimu kwa Klabu yetu. Tunafuraha kwa Ange kuungana nasi tunapojiandaa kwa msimu ujao," Levy alisema.

Ange Postecoglou anaridhi nafasi ambayo iliachwa wazi na Antonio Conte baada ya kutimuliwa mwezi Machi. Wakufunzi wa muda wawili wamesimama klabu hiyo tangu kufutwa kwa Conte.

Tottenham ilitamatisha mkataba wake na Conte baada ya Muitaliano huyo  kuishambulia klabu hiyo na wachezaji wake.

Hapo awali, Conte ambaye alikuwa akiisimamia klabu hiyo yenye maskani yake London tangu Novemba 2021 aliwakashifu wachezaji wake akiwaita "wabinafsi" baada ya kutoka sare ya 3-3 na Southampton.

Mnamo Machi 26, Tottenham kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti rasmi ya klabu hiyo ilitangaza kwamba meneja huyo mwenye umri wa miaka 53 ameondoka kwa makubaliano ya pande zote mbili.