West Ham yampiga marufuku shabiki aliyerekodiwa akinusa kokeini kwenye kipara cha mwingine (+video)

Taarifa ilisema klabu hiyo "imechukizwa" na tukio hilo.

Muhtasari

•West Ham imewapiga marufuku watu waliohusika kwenye video inayoonyesha shabiki mmoja akinusa kokeini kichwani mwa shabiki mwingine wakati wa mechi.

•Taarifa hiyo ilisema: “Klabu imechukizwa na yaliyomo kwenye video hiyo na imefanya upesi kuwatambua wahalifu hao.

Image: HISANI

Klabu ya West Ham imewapiga marufuku watu waliohusika kwenye video inayoonyesha shabiki mmoja akinusa unga mweupe unaoonekana kuwa kokeini kichwani mwa shabiki mwingine wakati wa mechi.

Taarifa ilisema klabu hiyo "imechukizwa" na tukio hilo, lililotokea wakati wa mchuano wa nyumbani kwenye Uwanja wa London Stadium.

Katika video hiyo, iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Alhamisi, shabiki mmoja alionekana akiweka unga mweupe kwenye kichwa cha shabiki mwingine wakati akivuta sigara ndani ya Uwanja wa London wa West Ham.

Shabiki mwingine alionekana akivuta unga huo kutoka kichwani mwa mwanamume huyo kipara aliyesimama mbele yake..

Mashabiki wengine pia walisikika wakimwambia "Fanya John, enda hapo" na "Je, bado umefanya hivyo John?"

Jamaa ambaye alikuwa akinusa unga huo mweupe alisema "Acha tupate" kabla ya kuvuta unga huo. Kisha alisikika akisema "Irons" - ambalo ni jina la utani la klabu.

Taarifa hiyo ilisema: “Klabu imechukizwa na yaliyomo kwenye video hiyo na imefanya upesi kuwatambua wahalifu hao.

"Kulingana na mtazamo wetu wa kutovumilia, maelezo ya wahalifu yalitumwa mara moja kwa polisi, na wote walipokonywa tikiti zao za msimu na kwa hivyo hawawezi kuingia London Stadium na kusafiri na kilabu kwa mechi za ugenini.

"Tukisubiri uchunguzi wetu wa klabu, hii inaweza kusababisha wahalifu kupigwa marufuku kwa muda usiojulikana. Hakuna mahali pa tabia ya aina hii."