Yaya Toure afunguka kuhusu kuwaagiza mababu kumlaani Pep Guardiola kwa kumdharau

Ajent wake wa zamani alidai Guardiola hatashinda Champions League tena kwa vile wazee wa Kiafrika walimlaani.

Muhtasari

•Dimitri Seluk alinukuliwa akidai kuwa laana ya kutofanikiwa katika Ligi ya Mabingwa ambayo mteja wake alimwekea Guardiola imeondolewa na kwamba watashinda kombe hilo msimu huu.

•Yaya Toure hata hivyo amejitenga na madai ya 'laana' na kuomba watu waache dhana potofu kuhusu uchawi wa Waafrika.

katika siku zake Man City.
Pep Guardiola na Yaya Toure katika siku zake Man City.
Image: HISANI

Mchezaji wa zamani wa Manchester City amejitenga mbali na madai ya kuomba usaidizi wa mababu wa Kiafrika 'African shamans' ili kumlaani meneja wa klabu hiyo Pep Guardiola kwa kuwabagua wachezaji wa Kiafrika.

Hivi majuzi, aliyekuwa ajenti wake Dimitri Seluk alinukuliwa akidai kuwa laana ya kutofanikiwa katika Ligi ya Mabingwa ambayo mteja wake alimwekea Guardiola imeondolewa na kwamba watashinda kombe hilo msimu huu.

Mwaka wa 2018, ajenti huyo kutoka Urusi alidai kwamba Guardiola hatashinda kombe hilo tena katika maisha yake ya soka kwa vile wazee wa Kiafrika walimlaani kwa madai ya kumtendea vibaya mchezaji huyo wa Ivory Coast.

Wakati akizungumza na gazeti la The Mirror hivi majuzi, Seluk hata hivyo alisema, "Nataka kuomba msamaha kwa jambo hili. Nadhani ni wakati wa kinyongo hiki kukoma - na najua kuwa Yaya anahisi vivyo hivyo kwa sababu hataki lolote ila mafanikio kwa City. Naweza kusema kwamba uchawi sasa umeondolewa na waganga - na kwamba nadhani City itashinda Ligi ya Mabingwa chini ya Pep."

Aliongeza "Wana nafasi kubwa ya kushinda mwaka huu. Lakini lolote litakalotokea, hakika wataishinda katika miaka mitatu ijayo. Unakumbuka wakati niliwahi kuikosoa City kwa kutompa Yaya keki mnamo siku yake ya kuzaliwa? Naam, ni siku yangu ya kuzaliwa mwezi huu na zawadi ninayotaka ni laana hii ikomeshwe. Kwa hakika, ni matumaini yangu kuwa City itashinda vikombe vitatu msimu huu."

Yaya Toure hata hivyo amejitenga na madai ya 'laana' na kuomba watu waache dhana potofu kuhusu uchawi wa Waafrika.

"Ajenti wangu wa zamani ananukuliwa na vyombo vya habari kuhusu 'laana'. Tafadhali msinihusishe na upuuzi huu na dhana potofu za uvivu kuhusu laana za Kiafrika," alisema kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mchezaji huyo wa zamani alibainisha kuwa Dimitri sio wakala wake tena na hayuko katika nafasi ya kuzungumza kwa niaba yake. Pia alivitaka vyombo vya habari kutowasiliana naye kuhusu masuala yanayomhusu.

"Kukuza dhana hizi potofu ni hatari," alisema.