Serena Williams abubujikwa na machozi akistaafu katika mchezo wa tenisi

Williams anamaliza taaluma ya miaka 27 ambayo ilileta ushindi mkubwa mara 23.

Serena Williams amestaafu kutoka mchezo wa tenesi
Image: BBC

Serena Williams amepungia mkono wa kwaheri mashabiki katika michuano ya US Open – huku kukiwa na hisia kali baada ya kupoteza mchezo wake dhidi ya Ajla Tomljanovic wa Australia katika usiku wa kusisimua huko New York.

Williams, ambaye anatimiza umri wa miaka 41 mwezi huu, amecheza mechi yake ya mwisho.

Anamaliza taaluma ya miaka 27 ambayo ilileta ushindi mkubwa wa mara 23 akiwa peke yake na kuonekana kuwa Mmarekani bora zaidi wa wakati wote.

Katika mchezo wake wa mwisho, Williams alipoteza kwa seti za 7-5 6-7 (4-7) 6-1 na akawa anatiririkwa na machozi baadaye huku akitoka uwanjani kwa kupungia mashabiki mkono.

Takriban kila mtu alisimama alipoondoka kwenye Uwanja wa Arthur Ashe - eneo la ushindi wake mkuu wa kwanza mwaka wa 1999 na ushindi mara tano bora zaidi katika historia ya taaluma yake.

Alipokuwa akipunga mkono wa kwaheri, wimbo wa pop wa Tina Turner ‘Simply The Best’ ulisikika kwa sauti ya juu ukiwa unavuma.

Alipoulizwa kama angefikiria tena kustaafu baada ya mchezo wake wiki hii, Williams alisema: ‘’Ninajihusisha sana na hili na kuwa bora zaidi. Nilipaswa kuanza mapema mwaka huu. Sifikirii hivyo, lakini huwezi kujua.’’

Williams alilemewa na hisia alipohojiwa katikati ya uwanja, akiishukuru familia yake, timu, umati na mashabiki wake kote ulimwenguni kwa usaidizi wao kwa miaka mingi.

‘’Namshukuru kila mtu aliye hapa, ambaye amekuwa upande wangu kwa miaka mingi, miongo mingi. Mungu wangu, miongo,’’ alisema Williams, ambaye alicheza mashindano yake ya kwanza ya kitaaluma akiwa na umri wa miaka 14 mwaka wa 1995.

‘’Lakini yote yalianza na wazazi wangu. Na wanastahili kila kitu. Kwa hiyo ninawashukuru sana. Na singekuwa Serena kama hakungekuwa na [dada] Venus, kwa hivyo asante, Venus. Yeye ndiye sababu pekee ambayo Serena Williams aliwahi kuwepo.’’