Elijah alikuwa miongoni mwa wakaazi wa Samburu ambao walifidiwa mamilioni ya pesa kwa kujeruhiwa na vilipuzi vilivyoachwa na wanajeshi wa uingereza walipokuwa wakifanya mazoezi katika eneo hilo. Wengi walipewa kiasi kikubwa cha pesa kama fidia baada ya kushinda kesi dhidi ya serikali ya Uingereza Julai mwaka wa 2002. Lorok alikuwa miongoni mwa watu 76 kati 228 waliofidiwa na idara ya ulinzi ya Uingereza ambapo familia nyingi zilifidiwa takriban euro elfu kumi. Lorok alijeruhiwa mgu alipokanyaga bomu la ardhini ambalo halikuwa limelipuliwa akiwa na umri wa miaka 12. Katika familia, yake zaidi ya watu 7 walifidiwa zaidi ya shilingi milioni kila mmoja lakini ni yeye alipewa kiasi kikubwa cha fidia kwa sababu baada ya kujeruhiwa, ililazimu madaktari waukate mguu wake.
Wakati watu walipofidiwa, wakaazi wengi waliopokea malipo hayo walianza kutumia vibaya pesa zao na Lorok anafahamika kwa kuyanunua magari manne kutumia pesa kwa siku moja. Aliingia jijini na binamu yake Lokwer na katika kampuni ya kuuza magari mapya walinunua magari mawili ya Mercedes benz, moja la Toyota prado na na lingine la Toyota cruiser. Inadaiwa siku hiyo walitumia takriban shilingi milioni 40 kununua magari na bidhaa zingine za kifahari walipokuja Nairobi. Kufikia Juni mwaka ufuatao wa 2003, Lorok hakuwa amesalia na hata shilingi moja na alikuwa tena amerejelea maisha yake ya hapo awali ya kuombaomba. Wakaazi wengi wa Samburu waliojua kuhusu kiasi cha pesa alizopewa walishangaa jinsi alivyoweza kutumia pesa hizo chini ya mwaka mmoja na kubaki bila chochote.
Kuna visa vya jinsi baadhi ya waliofidiwa pesa hizo walivyokuwa wakitumia ndege za kukodi kuja Nairobi na hata Mombasa kufanya raha na hata kuwaleta mamia ya makahaba kwa karamu kubwa kubwa makwao wakati walipokuwa na pesa. Lorok, inadaiwa wakati alipokuwa na pesa, alikuwa akiwalipa watu katika kituo chao cha kibiashara warejee nyumbani mapema ili waachie kituo kizima yeye na rafiki zake kufanya karamu kubwa zilizodumu usiku wote. Wakati mmoja alidaiwa kulaghaiwa shilingi milioni 10 na mfanyibiashara mmoja kutoka Laikipia aliyekuwa amemhadaa kwamba wangefungua biashara ya pamoja kwa kuanzisha shamba la ukulima wa mifugo na mazao huko Njoro. Msururu wa wanawake waliokuwa wakimfuata Lorok kila alikoenda uliwashangaza wengi na wakati mwingine katika msafara wake alikuwa na magari takriban 40 kwa wakati mmoja.
Mwaka wa 2019, Lorok alikuwa bado mjini Maralal akiwafanyia watu kazi za hapa na pale mashambani na hata wakati mwingine alitegemea huruma za watu kununuliwa chakula katika hoteli za vibandani mjini humo. Alipokuwa na pesa baadhi ya jamaa zake waliofaulu kumpunja mamilioni ya pesa walikuwa werevu na wakanunua vipande vya ardhi katika sehemu za Kisima, Lodosoit, Baragoi na Wamba –lakini wote hawataki kumuona tangu alipofilisika na walipogundua kwamba hakuwa na lolote la kuwapa.