'Mimi sio hasidi wa Man United,' Mourinho asema huku akirejea Old Trafford

Anaporejea leo Old Trafford kama mkufunzi wa Tottenham,Jose Mourinho amesisitiza kuwa yeye si hasidi wa Manchester United. Itakuwa ni vuta nikuvute leo ikiwa ndio mara ya kwanza Mreno huyo  kucheza dhidi ya United tangu klabu hiyo imtimue mwezi Disemba mwaka jana.

Mourinho aliiacha United ikiwa nambari 6 kwenye jedwali na furaha yake ni kwamba tangu atie guu katika kasri hiyo mpya, Tottenham imejizolea ushindi mara tatu.

Swali ni je, ni upi mustakabali wa wachezaji wa kutegemewa Tottenham?

Mshambulizi wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya Uswidi Zlatan Ibrahimovic,  mwenye umri wa miaka 38, anatarajiwa kugoma kurejea katika ligi ya Primia na badala yake kutia saini mkataba na klabu yake nyengine ya zamani ya AC Milan.

Meneja wa zamani wa Arsenal Arsene Wenger amesema Arsenal ingali kipenzi chake na yupo tayari kufanya mazungumzo na kaimu mkufunzi Freddie Ljungberg. Ljungberg, ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa Wenger alipoiongoza Arsenal Kati ya mwaka elfu moja kenda mia tisini na nane na mwaka  2007, alichukua nafasi hiyo kikaimu baada ya Unai Emery kupigwa kalamu juma lililopita.

Aidha amesisitiza kuwa angependa kuongea naye kabla ya timu yake kumenyana na Brighton hapo kesho.

Hayo yakijiri, Wenger amewataka wasimamizi wa ligi ya primia kumaliza ugomvi unaozingira matumizi ya kamera zitumiwazo uwanjani almaarufu VAR.

Naye msimamizi mwandamizi wa marefa kwenye ligi hiyo Mike Riley ametangaza kutotumiwa kwa kamera hizo na kuwaonya marefa dhidi ya suala hilo akidai mda mwingi hupotezwa kurejerea video hizo uwanjani.

Aidha, amesisitiza kuwa kamera hizo hazijawahi kutumika kwa takriban mechi 140 zilizosakatwa msimu huu.

Kwingineko, Real Madrid wanajiandaa kutuma ofa ya usajili kwa beki wa Napoli na timu ya taifa ya Senegal Kalidou Koulibaly, mwenye umri wa miaka 28, ambaye amekuwa akiwindwa kwa muda sasa na timu ya  Manchester United.