Mirengo ya Kieleweke na Tanga tanga yakutana Sagana

Rais Uhuru Kenyatta hii leo alikutana na viongozi kutoka mlima Kenya katika kaunti ya Kirinyaga kule Sagana.

Huu ni mkutano wa pili Rais Kenyatta ameandaa na viongozi hao wa mlima Kenya baada ya kuchaguliwa kuhudumu katika muhula wake wa pili.

Hisia mbali mbali zimezidi kuibuka kuhusiana na mkutano huo kwani chama cha Jubilee ambacho kwa sasa kimedaiwa kugawanyika kwa vipande viwili, upande wa tanga tanga na mrengo wa kieleweke, wote watahudhuria mkutano huo.

 Mrengo wa kieleweke ambayo kinapigiwa debe sana na mbunge wa zamani wa starehe Maina Kamanda na mbunge eneo la mji wa Nyeri Wambugu Ngunjiri wameonekana kuunga mkono ripoti ya BBI ambayo bado haijatolewa hii ni baada ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga kusalimiana almaarufu "handshake"

Tanga tanga kwa upande mwingine wameonekana kumpigia debe naibu wa Rais William Ruto, wakisisitiza kuwa Naibu huyo atawania kiti cha urais mwaka wa 2022, baada ya Rais Kenyatta kumaliza muhula wake.

Mrengo huo wa tanga tanga unaongozwa na mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung'wa na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na baadhi ya wengineyo.

Suala kubwa likibakia je, Rais Kenyatta ataweza kuleta umoja katika chama hicho cha Jubilee?