Mji wa Wuhan wafunguliwa baada ya miezi miwili kufuatia mkurupuko wa Covid-19

_111456837_060839902-1
_111456837_060839902-1
Mji wa China ambapo mlipuko wa virusi vya corona ulianza , Wuhan umefungua baadhi ya sehemu zake baada ya kutengwa kwa miezi miwili.

Makundi ya abiria yalipigwa picha yakiwasili katika kituo cha treni cha Wuhan siku ya Jumamosi. Watu wanaruhusiwa kuingia lakini sio kutoka, kulingana na ripoti.

Wuhan ambao ndiiu mji mkuu wa jimbo la Hubei uliandikisha visa 50, 000 vya maambukizi .Takriban watu 3000 walifariki katika jimbo hilo kutokana na virusi hivyo.

Lakini idadi hiyo imepungua kwa kiwango kikubwa , kulingana na takwimu za China.

Serikali siku ya Jumamosi iliripoti visa vipya 54 ambavyo inadai vilitoka nje ya nchi.

Huku ikiendelea kukabiliana na visa kutoka ughaibuni , China imetangaza marufuku ya muda kwa wageni wote hata iwapo wanamiliki Viza ama vyeti vya kuishi .

Pia imepunguza idadi ya ndege za China na zile za kigeni kusafirisha abiria mara moja kwa wiki, huku ndege hizo zikitakiwa kubeba asilimia 75 pekee ya abiria katika ndege moja.

Virusi hivyo vinadaiwa kuanzia katika soko moja la vyakula vya baharini ambalo lilikuwa likiuza wanyama pori kinyume na sheria.

Wakaazi milioni 11 wa mji huo walitengwa na ulimwengu tangu katikati mwa mwezi Januari , huku vituo vya kukagua magari vikiwekwa mbali na masharti makali yaliozuia maisha ya kawaida kuendelea.

Lakini barabara zilifunguliwa kuruhusu magari yanayoingia jioni siku ya Ijumaa kulingana na chombo cha habari cha Reuters.

Na vyombo vya habari vya serikali vilisema kituo cha ardhi cha treni kilifunguliwa siku ya Jumamosi na sasa treni zitaweza kuwasili katika vituo 17 vya reli mjini humo.

Mwanafunzi wa miaka 19 Guo Liangkai , ambaye alirudi mjini humo baada ya miezi mitatu , aliambia Reuters: Kwanza inanifurahisha kuona familia yangu tena.

''Tulitaka kukumbatiana lakini huu ni wakati maalum hatuwezi kufanya hivyo ama kufanya kitendo kama hicho''.

BBC