Mkenya afungwa jela kwa kuwatapeli wanyarwanda

Mjasiliamali raia wa Kenya amefungwa kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kuwatapeli Wanyarwanda wengi wao wakiwa ni vijana. Mahakama ya kigali imemhukumu Charles Kinuthia kuwatapeli maelfu ya vijana wa Kinyarwanda kwa kuandaa warsha feki mjini Kigali. Hata hivyo wakili wa Bwana Kinuthia amesema wataiomba serikali ya kenya iingilie kati.

Mafunzo feki yaliyoandaliwa na Bwana Kinuthia yalikuwa yamepangwa kufanyika tarehe 25 Juni katika ukumbi maarufu wa mikutano mjini Kigali - Kigali Convention Centre. Akitoa hukumu hiyo , jaji amesema kuwa kulikuwa na ushahidi ulioonyesha kuwa Bwana Kinuthia alipanga mkutano huo feki, na kuongeza kuwa kama mtu mwenye uzoefu wa kuandaa mikutano angeandika ujumbe wa maandishi wa kusahihisha makosa ya maelezo ya kikao hicho na kuituma kwa Wanyarwanda.

Mahakama pia imempata na hatia ya kutokuwa na utaalamu wa kutoa mafunzo ya ubunifu wa kazi.

Baadhi ya maelfu ya vijana waliojitokeza kwa ajili ya mafunzo hayo wameiambia BBC kuwa waliambiwa walipe dola 5 za usajili huku wakiahidiwa kuwa wangepewa dola 197 (sawa na 177,000 franga za Rwanda) kama marupurupu.

Hata hivyo mafunzo hayo hayakufanyika kwani Kinudhia na watu wake waliwaandikia watu kuwafahamisha kuwa viti havitoshi na kuwashauri kuwa wanahitaji kulipa gharama ndogo kulingana na mafunzo watakayopewa. Kulingana na ujumbe wa Kinuthia kulikuwa na aina tatu ya gharama za mafunzo, mafunzo ya ghalama ya dola 5, mafunzo ya dola 15 na dola 25 kulingana na uwezo wa mtu na mafunzo anayoyahitaji.

Mafunzo hayo yalisimamishwa kabla ya kuanza kwasababu idadi ya washiriki ilikuwa kubwa kuzidi kiasi kutokana na faida ya pesa waliyotarajia kupata ya $197. Inakadiliwa kuwa vijana 2500 walijiandikisha kushiriki mafunzo hayo feki ya ubunifu wa kazi.

Baadhi ya watu walizuiwa kuingia ndani ya jumba la mikutano kuhudhuria mafunzo hayo kwasababu hawakuweza kulipa huku wengine wakisikitika kubaini kuwa hawangepokea marupurupu ya dola 197 ambazo waliahidiwa kupewa kwa kuhudhuria mafunzo hayo.

Tukio hilo liliibua hisia kali katika miongoni mwa wanyarwanda ambao walielezea hasira yao kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, jambo lililosababisha maafisa wa usalama hususan Idara ya upelelezi ya Rwanda kuingilia kati.

Evode Kayitana, wakili wa Charles Kinuthia, ameiambia BBC kuwa hukumu iliyotolewa na mahakama haikuwa ya haki kwasababu waliweza kuthibitisha kuwa $197 ilikuwa ni thamani ya kozi ambayo wangeipata na sio pesa ambazo zingetolewa kwa washiriki wa mafunzo hayo.

" Na haiingii akilini ni kwa jinsi gani mahakama iliwaondolea mashtaka wanawake wawili raia wa Kenya na mwanamme mmoja Mnyarwanda also ambao ni waajiriwa na washtakiwa wenza wa Bwana Kinuthia na kumhukumu peke yake ", Amesema Bwana Kayitana.

Bwana Kayitana amesema mteja wake atakata rufaa juu ya uamuzi wa mahakama, lakini pia ataiomba serikali ya Kenya iingilie kati kwasababu anadhani ni swala la kidiplomasia.