Mkewe Rais wa Marekani Melania Trump atamatisha ziara ya siku mbili nchini Kenya

melanialeaveskenya
melanialeaveskenya
Mkewe Rais wa Marekani, Melania Trump, leo asubuhi ametamatisha ziara  yake ya siku mbili nchini Kenya.

Kwenye ziara hiyo ya kipekee katika mataifa manne barani Afrika, Mkewe Rais wa Marekani ametumia muda wake mwingi nchini Kenya kuliko mataifa mengine.

Ndege aliyosafiria Mkewe Rais wa Marekani iliondoka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta muda mfupi baada ya saa mbili asubuhi ambako aliagwa katika uwanja huo na mwenyeji wake Mama wa Taifa Margaret Kenyatta.

Bi Melania Trump anasafiri kwenda nchini Misri kwa mkondo wa mwisho wa ziara yake barani Afrika baada ya  shughuli nyingi nchini Kenya  ambako alifanya mashauri na mwenyeji wake katika Ikulu ya Nairobi, mbali na kuzuru maeneo mbali mbali katika jiji la Nairobi.

Mashauri kati yake na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta yalimulika masuala ya afya hasa maslahi ya akina mama na watoto, suala ambalo viongozi hao wawili wanalifuatilia kwa kina.

Mama wa Taifa Margaret Kenyatta ni mdhamini wa harakati za mageuzi katika sekta ya afya zinazoendeshwa na shirika la Beyond Zero huku Mkewe Rais wa Marekani Melania Trump  akiwa mwanzilishi na  mshirikishi wa harakati zinazotambulika kama “Be Best” ambazo zinakusudiwa kuboresha maslahi ya watoto.

Wakati wa mashauriano kati yao katika Ikulu ya Nairobi, Mama wa Taifa Margaret Kenyatta alimkabidhi Mkewe Rais Trump nakala ya Mfumo wa Mkakati wa shirika la Beyond Zero wa utendaji kazi katika kipindi cha mwaka wa 2018 hadi 2022. Mama wa Taifa alizindua Mkakati huo mapema mwaka huu.