Mkusanyiko wa habari kuu awamu hii - Radio Jambo

Viongozi wataka wenyeji wa Busia na Malaba kupimwa virusi vya corona. Hii ni kwa sababu ya kutangamana na madereva wa masafa marefu mpakani,  kuwepo kwa vichochoro Adungosi, Amung'ura, Mayenje na Alupe ni hatari.  Maeneo hayo yanatumiwa na watu kupenya kuingia Kenya na Uganda.

Tanzania imepuuzilia mbali ripoti kuhusu vipimo kwa madereva 19.  Madereva hao walipimwa Namanga na kupatikana kuambukizwa corona. Tanzania inasema iliwapima na kubaini kuwa hawajaambukizwa virusi. Tanzania inasema Kenya inatoa vipimo visivyo sahihi.

Kinara wa ODM Raila Odinga akutana na viongozi wa kike. Raila asema anashirikiana na rais Kenyatta kuhusu mipango ya nchi. Raila asema masuala ya jinsia yatashughulikiwa kwenye BBI.

Wawakilishi wadi sita kutoka Migori wataka doria kuwekwa mpakani. Wanahofia vichochoro vinavyotumiwa kuingia Tanzania vinahatarisha maisha. Wamekashifu mgogoro uliopo kuhusu usafirishaji wa bidhaa mpakani.

Mto Malimate umeanza kubadili mkondo na kutishia maisha ya watu. Wenyeji wa kijiji cha Kainuk wanahofia hali hiyo itasababisha janga. Wakulima wanasema zaidi ya ekari mia moja ya mashamba yao zimeharibiwa.

Baraza la magavana laelezea mipango ya kukabili corona. Kaunti ishirini na tatu nchini zimeathiriwa na COVID-19. Serikali za kaunti zimetenga shilingi bilioni tano kukabiliana na corona.