Mkusanyiko wa habari kuu awamu hii-Radio jambo

Chama cha walimu nchini KNUT kimeonya kuwa huenda kukawa na athari kubwa, iwapo shule zitafunguliwa mwezi ujao.

Katibu mkuu Wilson Sossion anasema mpango huo wa kufungua shule haufai kwa sasa na unapaswa kutathminiwa kwa makini sana. Waziri wa elimu George Magoha aliteuwa jopokazi la wanachama 9 kuunda mchakato wa kurejelewa kwa shughuli za masomo.

Tukisalia na  elimu, hivi karibuni wazazi watapokea mwongozo wa jinsi ya kuwasaidia wanao wanaposoma nyumbani. Katibu msimamizi wa elimu Mumina Bonaya anasema hii ni kwa sababu wamepokea ripoti kuwa wazazi wanasumbuka kuhakikisha wanao wanaendelea masomo wakiwa nyumbani baada ya shule kufungwa kutokana na janga hili la Corona.

Kwingineko, mamlaka ya NEMA imefunga kiwanda kimoja cha kusafisha mafuta ya kupikia katika eneo la South B kwa kutoa moshi yenye sumu ambayo huenda ikwadhuru wakaazi wa eneo hilo.

Aidha, baadhi ya wakaazi walikuwa wanalalamikia kukumbwa na maradhi ya kupumua kutokana na moshi hiyo.

Chama cha wiper kimekubali kufikia makubaliano ya kushirikiana na vyama vya Jubilee na KANU mara moja. Uamuzi huu uliafikiwa katika mkutano uliofanywa kupitia mtandao huku zaidi ya wanachama hamsini wa kamati kuu ya kitaifa wakikubaliana makubaliano hayo yatekelezwe.