Mkutano wa Umoja wa Mataifa: Uhasama kati ya Marekani na China kuhusu corona wajitokeza tena

Mvutano kati ya Marekani na China ulijitokeza mbele ya mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuilaumu China kwa kueneza virusi vya corona.

Alitaka China "iwajibishwe" kutokana na janga la corona.

Kati hotuba yake, Rais wa China Xi Jinping alisema nchi yake "haina nia ya kuingia katika Vita Baridi na nchi yoyote".

Uhusiano kati ya nchi hizo mbili zenye uwezo umezorota katika nyanja tofauti.

Mkutano wa mwaka huu mjini New York unaendeshwa zaidi kupitia mfumo wa kidijitali, huku viongozi wa duniani wakiwasilisha hotuba zilizorekodiwa.

Mfumo huo mpya ulimaanisha sarakasi za siasa za kimataifa zinazoshuhudiwa katika mkutano huo hazikuwepo. Kila nchi iliwakilishwa na mjumbe mmoja na kulikuwa na nafasi kidogo sana kwa nchi kujibizana.

Lakini kama ilivyotarajiwa, Rais Trump alitumia hotuba yake kushambulia mahasimu wake

China 'imeambukiza ulimwengu' - Trump

"Lazima tuwajibishe nchi ambayo ilileta pigo hili kwa ulimwengu - China," alisema.

"Katika siku za mwanzo kabisa za virusi China ilisitisha safari za ndege za ndani, huku ikiruhusu ndege kuondoka China na kuambukiza ulimwengu. China ililaani marufuku yangu ya usafiri dhidi ya nchi yao, licha ya kwamba walifutilia mbali safari za ndege za ndani na kuwafungia raia wake majumbani," aliongeza.

Rais Trump, ambaye rekodi yake kuhusu virusi vya corona inachunguzwa kwa makini wakati nchi hiyo inapolekea kwa uchaguzi, mara kwa mara amekuwa akilaumu Beijing kwa kuficha ukweli kuhusu virusi hivyo, akisema wangelisaidia kuzuia kusambaa kwa ugonjwa wa Covid -19. China imetaja tamko hilo kuwa uzushi usiokuwa na msingi wowote.

Idadi ya vifo vya corona nchini Marekani imefikia zaidi ya 200,000, ambayo ni ya juu zaidi duniani japo Rais Trump amekuwa akipuuza ugonjwa huo.

Hali ya taharuki imekuwa ikiongezeka kati ya Marekani na China katika masuala tofauti, ikiwemo biashara, teknolojia, Hong Kong na jinsi China inavyowatendea Waislamu walio wachache katika Mkoa wa Xinjiang.

Akizungumza muda mfupi baada ya kiongozi wa Marekani, Rais Xi alionya kuhusu hatari ya "mgongano wa ustaarabu".

"Tutaendelea kushughulikia tofauti na kutatua mzozo kati yetu na wengine kupitia majadiliano. Kamwe hatutaanzisha mchezo ambao hauna manufaa," alisema.

Katika tamko lake liliIotolewa kabla ya hotuba yake ya Jumanne, Rais Xi alitumia mbinu ya ustaarabu kushambulia Marekani, akisema "Hakuna nchi ina haki ya kusimamia maswala ya kimataifa, kuamua hatma ya wengine, ama kutumia manufaa yaliyopatikana kujiendeleza", jambo ambalo China yenyewe imelaumiwa kufanya na wakosoaji wake.

Pia katika hotuba yake, Rais Xi alisema China - ndio taifa kubwa duniani linalokuza gesi safi -na lengo lake ni kukomesha utoaji wa gesi chafu ifikapo 2030.

Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ambaye bila kutaja China au Marekani alisema ''lazima tufanye kila tunaloweza kuepusha vita baridi.''