Moi kuzikwa kichwa kikiangalia upande wa jua linapochomoza

Daniel Moi atazikwa kichwa chake kikiangalia upande jua huchomoza. Kulingana na mila za jamii ya Wakalenjini, rais huyo anayeheshimika sana angezikwa usiku, ili “aamke wakati wa jua linapochomoza”.

Hata hivyo kwa sababu Moi alikuwa mfuasi sugu wa dini ya kikristo, imani yake itaheshimiwa. Lakini hili halitazuia kufanyika kwa baadhi ya mila za jamii ya Wakalenjini. Katika mazishi hayo siku ya Jumatano wiki ijayo, baadhi ya mila zitaheshimiwa kwa sababu ya hadhi ya Moi katika jamii.

"Hii inamaanisha kwamba Moi atazikwa nyakati za alasiri kabla ya jua kutua. Hawezi kuzikwa wakati jua linapotua au kuchomoza. Hata hivyo atazikwa alasiri,” Mwenyekiti wa baraza la wazee wa Kalenjin John Seii aliambia alisema.

Mazishi yake yatazingatia mila za jamii ya Kalenjini na imani za Kikristo.

“Mila au tamaduni zimesalia thabiti lakini tunalazimika kuachana na baadhi ya mila hizo. Mazishi ya watu wetu siku hizi sio jambo letu tu au la kikabila bali ni swala la kitaifa,” Seii alisema.

Wazee wa jamii ya Tugen tayari wamechagua eneo litakalochimbwa kaburi la marehemu mzee Moi, ambalo litakuwa katika mkono wa kulia mbele ya boma lake la Kabarak. Moi alikuwa wa jamii ya Tugen kutoka kabila la Wakalenjin.

Kaburi lake litachimbwa na jeshi na kuna mipango ya ujenzi wa mnara kwa heshimu yake.

David Chepsiror, 77, rafikiye Moi na mwenyekiti wa Kanu, Uasin Gishu amesema lazima baadhi ya mila za Kalenjin zitekelezwe kwa sababu hadhi yake ilikuwa ya kitaifa, na hata ya kimataifa na pia alikuwa mfuasi sugu wa kikristo.

“Wakati wa kuzika, kichwa chake kitaangalia upande ambao jua huchomoza nyumbani kwake,” Chepsiror alisisitiza.