Moto ndani Jubilee: Jubilee yajitenga na mkutano wa wanachama wa Tangatanga mjini Naivasha

TUJU
TUJU
Chama cha Jubilee kimetuma taarifa kubainisha kwamba mkutano ulioandaliwa na viongozi wanaomuunga mkono naibu wa rais William Ruto huko naivasha haukuwa mkutano rasmi wa wajumbe wa chama hicho .

Katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju amesema mkutano huo haukuitishwa kwa mujibu wa sheria za katiba ya chama na hivyo basi maazimo yake sio msimamo rasmi wa Jubilee .

Taarifa ya Tuju inajiri baada ya  wabunge hao waliokutana Naivasha kuratibu maazimio kadhaa ikiwemo kuandaa mikutano sambamba ya BBI kama ile inayoandaliwa na wabunge wanaomuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga na wenzao wa kundi linalomuunga rais Kenyatta. Mkutano huo ulihudhuriwa na wabunge zaidi ya 173 . Chama cha Jubilee hata hivyo kimesema wanachama wake wana uhuru kuandaa mikutano kama hiyo kwani ni haki yao kikatiba .

Awali kundi hilo lilikuwa limesema litahudhuria mikutano ya BBI baada ya seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen  kuwaongoza  viongozi kadhaa wa tanga tanga katika mkutano wa Mombasa siku ya jumamosi, lakini sasa wamebadilisha msimamo na kuamua kuandaa mikutano tofauti katika maeneo mbali mbali ya taifa .