Mourinho agubikwa na simanzi baada ya kupoteza mechi ugani Old Trafford

mourinho (1)
mourinho (1)
Meneja wa Tottenham Jose Mourinho aligubikwa na simanzi katika himaya yake ya zamani ugani Old Trafford baada ya timu yake kufungwa mabao 2-1.

Bao la kwanza lilitiwa wavuni kunako dakika ya sita ya kipindi Cha kwanza na Marcus Rashford. United ilisalia kileleni katika mtanange huo ila ilipoteza nafasi nyingi kutikisa wavu. Kwingineko Liverpool ilitetea ubabe wake baada ya kuinyuka Everton 5-2.

Kocha wa Manchester United Solskjaer amesema anataka klabu hiyo kufanya maamuzi ya haraka katika dirisha la usajili, akiashiria kuwa mwenyekiti mtendaji Ed Woodward hakufanya maamuzi ya haraka mwishoni mwa msimu wa uliopita.

Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amefanya maamuzi ya kutofanya usajili wowote mwezi Januari licha ya klabu hiyo kuanguka kwenye safu ya ulinzi. Wakati huo huo, Manchester City na Barcelona wameingia katika kinyang'anyiro cha kutaka kumsajili mshambulizi wa Inter Milan na Argentina Lautaro Martinez mwenye umri wa miaka 22.

Atletico Madrid imekwepa adhabu kali baada ya Mashabiki wake kumpigia kelele na kumzomea Antoine Griezman walipomenyana na Barcelona kwenye kombe la La liga. Shirikisho la soka la Uhispania limesema litaipiga faini Atletico kima cha pauni 250 kwa kuzua vurugu uwanjani.

Mbio za nyika za kinadada zilizoratibiwa kufanyika mwaka 2020 huko Tokyo zimebadilishwa na hivyo zitaandaliwa mjini Sapporo. Waandalizi wamebadilisha tarehe ili kuwapa wanariadha wengi fursa ya kushiriki. Mbio hizo zimesogezwa kutoka Agosti tarehe 2 huku wanaume nao wakitarajiwa kukimbia siku ya mwisho ya mbio hizo ilivyo desturi.

Mbio hizo zimehamishwa kutoka Tokyo kutokana na hali ya joto jingi nchini humo.

Timu ya raga ya kinadada itacheza leo jioni mwendo wa saa moja kasorobo usiku dhidi ya Afrika Kusini nchini Dubai. Kinyume na ilivyokuwa katika msimu uliopita wengi wa wachezaji ambao hawakucheza wamo kambini wakiongozwa na mkufunzi Paul Feeney ambaye ameahidi kuandikisha ushindi msimu huu.