Kupitia barua iliyoandikwa na kaimu katibu wa tume hiyo Millicent Okatch, Muigai ametakiwa kufika mbele ya tume hiyo Juni tarehe 26 saa nne asubuhi. Endapo atakosa kufika mbele ya tume hiyo kama ilivyoagizwa, Muigai atajitia katika hatari ya kushtakiwa kwa ukiukaji wa agizo hilo. Amesema hana nia ya kupuuza agizo hilo .
Katika wimbo huo Ino Migunda – neno linalomaanisha ‘mashamba hayo’ Muigai ameweza kuzua mjadala kuhusu uhalali na njia inayotumiwa kuwafurusha watu kutoka mashamba yanayodaiwa kumilikiwa na serikali. Wimbo kufikia sasa umechezwa mara 650,000 na watu katika Youtube.
“Shamba hili siku moja litagawanywa kwa njia iliyo sawa kwa sababu haliwezi kukabdhiwa binadamu. Boma moja Kisumu litakuwa mashakani na ukemi utasikika kutoka Nyahururu hadi Kabarak’ amesema msanii huyo katika wimbo huo wake.
Kulingana na NCIC, maneno hayo ni ya uchochezi na yanatishia utangamano wa kitaifa na uthabithi wa nchi
Ni mara ya pili kwa mwanamuziki huyo kutikisa ndimi za watu kupitia muziki wake baada ya wimbo wake mwingine kwa jina Tukunia kukosolewa na kusifiwa na watu alipolalamikia ukosefu wa maendeleo katika eneo la Mlima Kenya na kumtwika lawama rais Uhuru Kenyatta kwa hali hiyo.
Katika wimbo huo, Njoroge anamksoa rais Kenyatta kutokana na jinsi anavyomtenga naibu wake William Ruto akifananisha hali hiyo kama kuavya mimba ya miezi saba. Hata hivyo, katika mahojiano na gazeti la The Star, Njoroge amekana kwamba alilipwa na Ruto kuutoa wimbo huo.