Mswada wa punguza mzigo wapata pigo kubwa Garissa

garissa
garissa
Viongozi kutoka kaunti ya Garissa wameapa kukataa mswada wa 'Punguza mzigo' na kusema kuwa wataunga mkono ajenda ya BBI .

Wakizungumza katika mji wa Sankuri siku ya jumatatu wakati wa ziara ya maendeleo, viongozi hao walisema kuwa wamepitia mapendekezo hayo ya Punguza mzigo na wamegundua kuwa mswada huo haujashughulikia maswala yanayoathiri watu katika kaunti hiyo ya Garissa.

 Gavana Ali Korane alisema kuwa wanasubiri kwa hamu mapendekezo ya BBI, hii ni baada ya wao kutoa maoni yao.
Gavana huyo alieleza zaidi kuwa sababu ya kuunga mkono BBI ni kwamba mapendekezo yao yalitokana na agenda kuu ya Rais Uhuru Kenyatta.

Gavana huyo aliwasihi wanasiasa na wakaazi waepuke siasa za mapema na badala yake walenge nguvu zao kwa kuzidisha maendeleo.

Mbunge wa Balambala Omar Shurie alisema kuwa hakuna kitu chochote kizuri katika mswada unaopendekezwa na Ekuru Aukot wa chama cha Thirdway alliance.

Shurie aliwataka wajumbe katika bunge la kaunti hiyo ya Garissa kutupilia mbali mswada huo pindi tu utakapowasilishwa bungeni.

Mwezi uliopita, wajumbe wengi wakiongozwa na kiongozi wa wengi Mohamed Gabow na spika katika bunge hilo Ibrahim Abass waliahidi kuwa watapitisha mswada huo.

Wawili hao walihutubia waandishi wa habari baada ya kumsikiliza Ekuru Aukot akielezea maelezo yake.

Kwa sasa kaunti 14 yamekataa kupitisha mswada wa Punguza mzigo kwa msingi kuwa inalenga kupunguza idadi ya wawakilishi.