Mtafaidi nini mkiniua? Maisha yangu yamo hatarini, Moses Kuria asema

moses kuria
moses kuria
Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amesema maisha yake yamo hatarini kutokana na msimamo wake wa kisiasa. Kuria aliyasema hayo Jumanne Juni 2, baada ya kutoka kwenye mkutano wa Jubilee uliofanyika Ikulu.

Kupitia kwa ukurasa wake wa Facebook, Kuria alisema hataogopa lolote kwa sababu kile anafanya ni kuzungumza ukweli.

"Sasa mtafaidi nini mkiniua? Kwani mimi ndio nitakuwa wa mwisho kuwaambia ukweli?" Kuria alisema. 

Mbunge huyo aliandika majina ya viongozi wengine wa kisiasa ambao waliuawa katika kile kilionekana kama mizozo ya kisiasa na serikali.

Wanasiasa JM Kariuki, Tom Mboya na Pio Gama and Pinto waliuawa katika malumbano ya kisiasa yaliyohusishwa na rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta.

Mzee Jomo ndiye babake rais wa sasa Uhuru Kenyatta huku Kuria naye akiwa ndiye mbunge wa nyumbani kwa Uhuru Gatundu.

Kuria amekuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Rais Uhuru Kenyatta huku akimpigia debe Naibu Rais William Ruto.

Mbunge huyo wa Gatundu Kusini ni mmoja wa wabunge 212 waliohudhuria kikao cha Ikulu Juni 2 ambapo inaarifiwa Rais aliwazomea sana.

Swali kuu kwa wananchi na ambalo wanaulizana kila kuchao je, kunani?