Muhubiri amekamatwa kwa tuhuma za kumuoa msichana mdogo

Muhubiri mmoja wa kanisa la new apostlic kutoka kata ya Bukhayo mashariki kaunti ndogo ya Nambale kaunti ya Busia amekamatwa kwa tuhuma za kumuoa msichana mdogo na kumpachika mimba.

Muhubiri huyo Fredrick Okwero Dindi mwenye umri wa miaka 38 kutoka Ekisumo alikamatwa na chifu wa kata hiyo Gerishom Pate kwa ushirikiano na maafisa wa polisi wa utawala wa Mungatsi baada ya kumuoa msichana huyo yatima kutoka kijiji cha Ibokolo kaunti ndogo ya Butere kaunti ya Kakamega miaka mitatu iliopita alipokuwa na umri wa miaka 14.

Msichana huyo alipachikwa mimba ya kwanza na muhubiri huyo na kuzaa kwa njia ya upasuaji huku mtoto akifariki muda mfupi baada ya kuzaliwa na sasa yuko na mimba ya pili ya miezi sita.

Muhubiri huyo ambaye bibi wake wa kwanza alienda kwao na kumuachia watoto saba ameomba msamaha kutokana na kitendo hicho akidai kuwa hakujua umri kamili wa msichana huyo alieletewa na mwanamke mmoja licha ya kuonekana mdogo kimwili.

Leonard Acharry Ojiambo