Mutahi Kagwe: Hatuwezi kuwafunga jela wanaokana kuwepo kwa COVID 19

Serikali haiwezi kuwafunga jela watu wanaokana kuwepo kwa ugonjwa wa corona, amesema waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

Kagwe amesema wanaokana kwamba ugonjwa huo haupo basi wanafaa kuungoja. Katika siku ambayo Kenya imesajili vifo vingi  vya watu wengi kwa siku moja kwa ajili ya virusi hivyo -12 , Kagwe amesema  sasa ni jukumu la kila mkenya kujitunza mwenyewe.

"... Itawachukua muda gani wafahamu kwamba ugonjwa huo upo, iwapo mtu anapinga hilo basi hakuna  unachoweza kufanya'

Kenya  leo imesajili  idadi ya juu ya watu walioaga dunia kwa siku moja kutokana na ugonjwa wa corona baada ya watu 12 kuaga dunia.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe amesema wote walioaga dunia ni kutoka Nairobi. Amesema watatu waliaga dunia wakiwa nyumbani ilhali waliosalia walifariki wakiwa hospitalini.

Kagwe ameongeza kwamba visa 189 vya ugonjwa huo vimeripotiwa nchini katika saa 24 zilizopita na kufikisha jumla ya visa hivyo nchini kuwa  10,294. Visa hivyo ni kutoka kwa sampuli 1,205  na kufikisha jumla ya sampuli zilizopimwa hadi sasa kuwa  216,242.

Kati ya visa hivyo vipya, 106 ni  vya wanaume ilhali 83 ni wanawake.

Nairobi inaendelea kuwa kaunti inayoongoza kwa idadi ya visa vingi baada ya watu 147 kupatikana na virusi hivyo. Kaunti nyingine ni

Kiambu 20, Machakos 11, Kajiado 5  na Mombasa 2.Waziri Kagwe amesem sampuli nyingine zilizokusanywa leo hazijapimwa kwa sababu ya changamoto ya kielektroniki .