Mutyambai achukuwa hatua dhidi ya polisi waliompiga kinyama mwanafunzi wa JKUAT Jumatatu

JKUAT
JKUAT
Inspekta mkuu wa polisi Hillary Mutyambai ameagiza kitengo cha maswala ya ndani ya polisi kuchunguza maafisa wa polisi walionaswa kwenye video wakimpiga kinyama mwanafunzi wa chuo kikuu cha JKUAT.

Kwenye taarifa siku ya Jumanne, Mutyambai imekipa kitengo hicho saa 24 kuwasilisha ripoti kamili ya udhalimu huo wa polisi.

"Tumetamaushwa na video inayozungushwa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha maafisa wa polisi wakitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya mwanafunzi wa JKUA siku ya Jumatatu,” Mutyambai alisema.

Maafisa hao walikuwa wameitwa kutuliza ghasia baada ya wanafunzi wa chuo hicho kuzua rabsha na kufunga barabara kuu ya Thika. Wanafunzi hao walikuwa wamekabiliana na polisi kutoka kituo cha Juja kwa takriban saa mbili hatua ilio athiri shughuli za usafiri mjini Thika.

Wanafunzi hao walikuwa wanashtumu maafisa wa polisi kwa kukosa kuwapa ulinzi dhidi ya wahalifu. Walidai kuwa wahalifu waliojihani kwa visu wamekuwa wakiwahangaisha hata mapema saa kumi na mbili za jioni na kuwaibia pesa, simu na hata vipakatalishi.

Chuo hicho kilifungwa kupia notisi kutoka kwa kaimu Naibu Makamu wa Chansela wa chuo hicho anayesimamia maswala ya elimu.

Muungano wa wanafunzi wa chuo hicho kupitia rais wa muungano huo Clinton Osoro na katibu mkuu Bruce Akach ulisema wahalifu walishambulia wanafunzi wawili majuma mawili yaliopita na kuaacha na majeraha mabaya ya visu.

Inspekta mkuu wa polisi alionya kwamba hatua za polisi kutuliza ghasia hazifai kuwa za kudhulumu mtu bali zinafaa tu kuwa za kudumisha sheria na kuhakikisha washukiwa wanafikishwa mahakamani.