Mwanafunzi wa chuo kikuu abakwa, auawa nyumbani kwake Kasarani

Mwanafunzi mwenye umri wa miaka 24 wa chuo kikuu cha Kisii alibakwa kabla ya kudungwa kisu hadi akafa katika makaazi yake mtaani Kasarani.

Usiku kabla ya kifo chake, Leah Momanyi aliwasili kwake saa 8 usiku na kuelekea chumbani kwake iliyoko ghorofa ya pili, hayo ni kulingana na majirani na bawabu.

Msimamizi wa jumba hilo aliambia maafisa wa upelelezi wa Kasarani kuwa alisikia Momanyi akipiga mayowe usiku saa 11.35 Novemba 8, lakini hangebaini haraka kulikotoka mayowe hayo.

Majirani wanasema kwamba walipigia simu polisi kutoka kituo cha Sandton, ambacho ni mita 50 tu kutoka jumba hilo saa 2 asubuhi lakini hawakutambua kulikotokea kelele hizo usiku huo.

Mwili wake ulipatikana na anayedaiwa kuwa mpenzi wake siku 2 baadaye.

"Jumapili 10/11/2019, saa 6 asubuhi, mpenzi wake anadai kuwa alitoka kwao na alipofungua mlango kwa ufunguo wake, alipata mwili wa Leah kitandani huku damu ikiwa sakafuni, pia kulikuwa na kisu kwenye sakafu," taarifa iliyoandikishwa kwa polisi ilisema.

Alipopata mwili huo wa Leah, alimjulisha binamu yake ambaye anaishi karibu na eneo hilo.

Daktari walipofanyia mwili huo upasuaji katika hospitali ya chuo cha Kenyatta, walibaini kuwa mwendazake alibakwa kabla ya kunyongwa na kudungwa kisu, mjomba yake Joseph Chacha alisema.

Aidha Chacha alisikitikia utepetevu wa polisi kulishughulikia jambo hilo kwa upesi, huku akisema kwamba uchunguzi wao unaendeshwa kwa mwendo wa pole.

Kulingana na mjomba wake, mwanafunzi huyo anayesomea teknolojia na mawasiliano, alikuwa amekuja Nairobi kutafuta karo za mwaka wa tatu chuoni na alikuwa ameajiriwa katika duka moja la kuuza mvinyo.