Mwanaharakati Omtatah ashinda katika kesi ya kuwashtaki wabunge

Mahakama kuu imemruhusu mwanaharakati Okiya Omtatah kuweka tangazo kwenye gazeti la majina ya wabunge aliowashtaki

Katika kesi hio, Omtatah anapinga marupurupu ya nyumba waliojipatia wabunge na anaitaka mahakama kusitisha malipo hayo akihoji kuwa yako kinyume cha sheria.

Omtatah ameiambia mahakama kwamba itakua vigumu kwake kuwapa wabunge hao 400 notisi ya kuwashtaki mmoja baada ya mwingine, na akaitaka mahakama kumruhusu kuweka notisi hio gazetini.

Jaji James Makau aliruhusu ombi hilo akisema kuwapa wabunge hao notisi kila mmoja ni kibarua kigumu ambacho kitachukua muda mrefu.

Mwanaharakati huyo pia ameishtaki kamati ya huduma za umma PSC na maspika wa mabunge yote mawili.

Anahoji kuwa PSC na bunge hazina mamlaka ya kisheria kutathmini mishahara ya wabunge.

Omtatah pia anasema iwapo mahakama haitasitisha malipo hayo, mlipa ushuru atakua katika hatari ya kupoteza viwango vikubwa vya pesa.

Omtatah alikua amewashtaki wabunge wote na maseneta kwa 'kupokea marupurupu ya nyumba kinyume cha sheria'.

Pia alikua ameishtaki hazina ya kitaifa, mthibiti wa bajeti na mwanasheria mkuu.

“Marupurupi hayo ya nyumba ya shilingi elfu 250 kwa mwezi, yatawagharimu walipa ushuru shilingi milioni 104 kila mwezi sawia na shilingi bilioni 1.2 kila mwaka,” Omtatah amesema.