Mwanamke afichua kuwa ilimbidi kuuza nywele zake ili alishe wanawe

"Kijana wangu wa miaka 7 Kaliyappan alikuja kutoka shuleni na kuomba chakula. Kisha kaanza kulia kwa sababu ya njaa," amesema Prema Selvam.

Lakini mama yake mwenye umri wa miaka 31, ambaye anaishi eneo la Salem mji wa Tamil Nadu, nchini India, hakuwa na chochote cha kumpa na alihisi kukosa matumaini kabisa.

Nini hasa kilichotokea, Ijumaa Januari 3. Hakuwa na chochote cha kupika.

Baada ya siku kadhaa za matukio kama hayo, Prema alikuwa amefikia kiwango kibaya na kuamua kuchukua hatua ambayo haikuwa ya kawaida na watu wengi wa jamii yake wakaitikia wito.

"Sikuwa na chochote cha kuipa familia yangu. Nilisikita sana. Na nikaanza kufikiria kuna haja gani ya kuishi wakati siwezi kulisha watoto wangu?" aliiambia BBC.

Prema hakuwa na mali, vito vya thamani, ama hata vyombo vya nyumbani ambavyo vingeweza kubadilishwa kwa pesa.

"Sikuwa hata na noti ya rupia 10 (senti 14)," amesema. "Nilikuwa na ndoo ndogo tu za plastiki."

Kisha akagundua kwamba kuna kitu anachoweza kuuza.

"Nilikumbuka duka ambalo nilikuwa nikinunua nywele. Nilienda hapo na kuuza nywele zangu zote kichwani kwa rupia 150 ($2)," Prema amesema.

Nywele za kubandika za binadamu huuzwa kote ulimwenguni na India ndiyo inayouza kiwango cha juu cha nywele hizo nje ya nchi.

Baadhi ya waumini wa kihindi hutoa nywele zao kwenye mahekalu baada ya kujibiwa maombi yao.

Wanaohusika na biashara hiyo hununua nywele hizo na kuziuza nje ya nchi.

-BBC