Mwanamke aliyekuwa amehukumiwa kwa kosa la kumuua rafikiye kwa sababu ya mpenzi wake mzungu aachiliwa huru

Naibu Jaji mkuu Philomena Mwilu ajumuika na wafungwa katika gereza la wanawake la Lang'ata
Naibu Jaji mkuu Philomena Mwilu ajumuika na wafungwa katika gereza la wanawake la Lang'ata
Mwanamke raia wa Rwanda aliyekuwa amehukumiwa kufungo cha maisha gerezani mwaka 2018 ameachiliwa huru na mahakama ya rufaa.

Antoinette Uwineza alikuwa amehukumiwa kwa kosa la kumuua rafikiye aliyekuwa mja mzito kwa sababu ya mpenzi raia wa Uingereza.

Mwaka 2018 Jaji Jessie Lessit alimpata na hatia Uwineza kwa mauaji ya Winne Uwambae ambaye pia alikuwa raia wa Rwanda na ambaye alikuwa rafiki yake wa karibu.

Jaji Lessit alikuwa amemhukumu kifungo cha maisha lakini siku ya Ijumaa mahakama ya rufaa ilimuachiliwa huru bila masharti yoyote.

Uwineza alishtakiwa Februari 16, 2013 kwamba katika Saharan Lodge iliyoko barabara ya Duruma mjini Nairobi alimuua Winne aliyekuwa na mimba ya miezi saba.

Alishtakiwa pamoja na washukiwa wengine wawili lakini wale wengine waliachiliwa huru na yeye pekee aliyepatikana na hatia ya mauaji.

Polisi walikuwa wamedai kwamba wawili hao walikuwa wakipigania mwanamume huyo mzungu aliyekuwa amempuuza Uwineza na kumpenda Winnie.

Kupitia wakili wake John Swaka , Uwineza alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Lessit akishikilia kwamba hakuwa na hatia.

Katika uamuzi uliyotolewa siku ya Ijumaa, majaji Martha Koome, Hannah Okwengu na Fatuma Sichale walikubali rufaa yake na kusema kwamba ushahidi uliyotumiwa kumhukumu haukutosha vigezo vinavyotakikana.

Mahakama ya rufaa ilisema kwamba upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha sawa sawa kwamba Uwineza alimuua Winnie.

Majaji hao hata hivyo walikubali kwamba Winnie aliuawa kwa kunyongwa lakini lilikuwa jukumu la upande wa mashtaka kuleta ushahidi wa kutosha kudhihirisha mahakama kwamba ni kweli Uwineza ndiye aliyemuua raifikiye.