Kidosho milionea wa miaka 28, ni miongoni mwa walioidhinishwa kuhudumu NCIC

Peris Nyutu
Peris Nyutu
Mrembo mwenye mihela si haba ukipenda milionea akiwa tu na umri wa miaka 28 ni miongoni mwa watu walioidhinishwa na bunge kuhudumu katika tume ya uwiano na maridhiano NCIC.

Peris Nyutu aliyezaliwa mwaka 1991 na kufuzu kutoka chuo kikuu cha Nairobi na shahada ya unasheria, aliiambia kamati iliyokuwa ikimhoji kuwa anamiliki mali yenye thamani ya shilingi milioni 23.

Kulingana na hati iliyowasilishwa kwenye tume ya maridhiano na uwiano, Nyutu amehudumu kama mkurugenzi katika bodi ya kitaifa ya unyunyiziaji maji mashamba tangu mwaka wa 2016.

Alipewa tuzo ya OGW (Order of the Grand Warrior) Kutokana na juhudi zake katika kuongoza kikundi cha Warembo na Uhuru ambacho kilimpigia kampeni Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Wabunge pia waliidhinisha uteuzi wa Samuel Kobia kuwa mwenyekiti, Philip Okundi, Abdulaziz Farah, Danvas Makori, FatUma Tabwara, Dorcas Kedogo  na mwenyekiti wa zamani wa bodi ya Kerio Valley Development Authority Samuel Kona.

Wanane hao walipendekezwa na Rais Uhuru Kenyatta kuhudumu katika tume hiyo ili kuimarisha juhudi za kuleta maridhiano na uwino na kudumisha umoja wa kitaifa pamoja na kushauri serikali.

Wabunge waliwasihi wanachama hao wapya kudumisha hadhi ya taifa.

Kiongozi wa walio wachache bungeni, John Mbadi alisema kwamba NCIC lazima iwajibikie nidhamu katika jamii.

"Nadhani ni muhimu tume hii kuleta uwiano na maridhiano katika taifa hili," Mbadi alisema.