Mwenda sasa anataka kufidiwa na serikali baada ya unyama huo ambapo alilazimika kusalia nje ya kituo cha polisi huku yeye pamoja na mwili wa mkewe katika jeneza wakinyeshewa na mvua.
Amewasilisha kesi katika mahakama kuu ya Meru akidai haki zake za kimsingi zilikiukwa kwa ajili ya yote aliyopotia nje ya kituo cha polisi cha Kianjai
Anaitaka mahakama kuamuru kwamba polisi walimfanyia ukatili licha ya yeye kutii kanuni za kukabiliana na COVID 19 ambazo serikali ilikuwa imetangaza.
Ameeleza jinsi yeye pamoja na waombolezaji wengine 31 walivyopewa idhini ya kusafiri kutoka Malindi hadi Meru kwa mazishi ya mke wake Faith Mwende aliyefariki Mei tarehe 24 mwaka huu lakini walipofika katika soko la Keeria walisimamishwa na polisi na waombolezaji hao 31 wakiwemo watoto wake wawili kuagizwa kurejea Malindi.
Kikosi cha polisi waliojihami kisha kilimuagiza Mwenda kuabiri gari la polisi pamoja na jeneza na mkewe na kumpeleka katika kituo cha polisi cha Kianjai. Amesimulia jinsi wakati wa usiku alivyowarai polisi kumsaidia kuusafirisha mwili wa mke wake hadi kijijini mwao ,umbali wa kilomita tano lakini walikataa.