Mwanaume mmoja akatakata watu wawili mjini Awendo

Polisi wanamtafta mwanamume mmoja aliyekuwa amemridhi mkewe baada ya kuwakatakata na panga mashemeji zake na kuwauwa papo hapo.

Jaoko Anyiko anasemekana kutembea kwa zaidi ya kilomita 20 ilikufika nyumbani kwa mpenziwe kijijini Orandi, Awendo akitoka Uriri.

Kulingana na msemaji wa polisi Joseph Nthenge, Bwana Anyiko alijaribu kumchukua mwanawe kwa amani ila mambo yakashindikana kwani Antony Otieno, 45, na Charles Obondo, 32, walimfukuza.

Jaoko alingia kwenye shamba la miwa lililokuwa karibu na baada ya wawili hao kumfuata walipatana na mauti yao kwani waliambulia kukatwa katwa na panga.

 "Mwanamke huyo amekuwa na uhusiano na Jaoko kwa muda sasa ila mzozo ulianza wakati mwanamke huyo alisema kuwa alikuwa anahitaji kuridhiwa na shemeji zake kama ilivyo kwa desturi za mila ya kijaluo," Victor Ojowi mzee wa kijiji alisema.
Wanakijiji wengine wanasema kuwa wawili hao wamekuwa na mzozo wa kifamilia tena walivunja ndoa yao mwezi Oktoba mwaka uliopita baada ya kupigana.

Kulingana na mila za kijaluo, mwanamke mjane anapaswa kuridhiwa na mwanaume spesheli, 'Jater' ambaye anapaswa kulala nyumbani kwa mjane huyo pamoja na kuacha virago vyake huko huku pia wakishiriki ngono.

"Anyiko alipouliza kuhusu bintiye aliambiwa kulingana na mila na desturi, mtoto anapaswa kubaki na mamaye na kubakia kuwa wa marehemu. Jambo hilo lilimuudhi sana," Anyango mmoja wa wanakijiji alisema.

Polisi wa Migori Bwana Nthenge alisema kuwa maiti za wawili hao ilipelekwa chumba cha kuhifadhi maiti cha Rapcom huku pia oparesheni za kumtafta muuaji huyo zikianza mara moja.